Habari za Kitaifa

Sioni nikipata haki hapa, alia Gachagua akitaka majaji wajiondoe katika kesi yake

Na RICHARD MUNGUTI October 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAWAKILI wa Naibu Rais aliyetimuliwa ofisini, Bw Rigathi Gachagua, Alhamisi waliwataka majaji watatu wa Mahakama Kuu wajiondoe kusikiliza kesi alizowasilisha akiwalaumu kwa upendeleo.

Wakiongozwa na wakili Paul Muite na Dan Maanzo, mawakili wa Gachagua walitoa madai kwamba baadhi ya majaji wana ukuruba na viongozi wa serikali na bunge na kwamba mbunge huyo wa zamani wa Mathira hawezi kupata haki.

Hatua hiyo ilijiri siku moja baada ya majaji hao kuzima malalamishi ya Bw Gachagua kwamba hawakuteuliwa kwa njia inayofaa.

Bw Gachagua alikuwa amehoji kuwa Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu hakuwa na mamlaka ya kuteua jopo la majaji kusikiliza kesi. Majaji waliamua kwamba akiwa msaidizi wa Jaji Mkuu, Jaji Mwilu hakukosea kuwateua kushughulikia kesi hiyo.

Majaji wa Bunge la Kitaifa, Mwanasheria Mkuu na Maspika wa Bunge na Seneti wakiongozwa na Profesa Githu Muigai walipinga ombi la majaji kujiondoa wakisema halikuwa na mashiko.

Hadi tulipoenda mitamboni jana, majaji walikuwa wakiendelea kusikiliza ombi la kujiondoa.