Habari za Kitaifa

Sitaruhusu Ruto agawanye Mlima, aapa Gachagua

Na GEORGE MUNENE January 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua Ijumaa, Januari 3, 2025 alimsuta Rais William Ruto na kuapa kutomruhusu kugawanya eneo la Mlima Kenya.

“Rais alitaka kugawanya eneo hili mara mbili, Mashariki na Magharibi lakini nilimkataza, ndiyo maana alinitimua serikalini,” alisema.

“Sababu iliyotufanya tukosane na Rais ni pale alipojaribu kugawanya Mlima. Nilikataa jaribio lake na akahakikisha nimetimuliwa serikalini,” alisema.

Alionya kuwa Mlima Kenya ‘utaisha’ ikiwa wakazi watakubali kugawanywa.

“Nguvu zetu ni umoja wetu na tunapaswa kubaki imara,” alisema.

Akizungumza wakati wa ibada ya mazishi ya marehemu Eric Mutugi, 41, mtoto wa aliyekuwa Seneta wa Embu Lenny Kivuti katika uwanja wa michezo wa Shule ya Sekondari ya Kanyuambora huko Mbeere, Bw Gachagua aliapa kuwa majaribio ya Rais kugawanya Mlima yatapingwa vikali.

Gachagua alisisitiza kuwa kufuatia kuondolewa kwake, Mlima sasa una umoja hata kuliko hapo awali.

Aliwaambia wakazi wa Mlima Kenya wasiwe na hofu kuhusu kuondolewa kwake, akiahidi kuwapa mwelekeo wa kisiasa mwezi huu.

Bw Gachagua alisema amewasikiliza wazee, viongozi wa makanisa, wataalamu na wafanyabiashara na atatoa taarifa ya kina ya kisiasa.