Habari za Kitaifa

Soipan Tuya: Sina ujuzi mwingi kwenye masuala ya Ulinzi lakini nitajifunza

Na MWANDISHI WETU August 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAZIRI Mteule katika Wizara ya Ulinzi Roselinda Soipan Tuya ameambia kikao cha Bunge kwamba anafahamu hana ujuzi mkubwa katika idara ya ulinzi, lakini yupo radhi kujifunza na kutekeleza wajibu wake iwapo ataidhinishwa.

Akijibu maswali katika kikao cha kupigwa msasa kubaini ufaafu wake katika wadhifa huo kilichoongozwa na Spika Moses Wetang’ula, Bi Tuya alisema yeye ni mtu anayejifunza mambo upesi na kwamba ana uwezo mkubwa wa kushirikiana na wengine ili kufanikisha majukumu.

“Mimi hushika mambo upesi na hushirikiana sana kwa karibu na wenzangu. Kuna mengi ambayo nitahitaji kujifunza kuhusu masuala ya ulinzi…nitafahamu vizuri hali ya mambo bila kuingilia majukumu ya wanajeshi. Hilo nawahakikishia,” akajibu.

Bi Tuya, kama wenzake waliotangulia kupigwa msasa Alhamisi, alisema utajiri wake umeongezeka kutoka Sh156 milioni alizofichua alipopigwa msasa 2022, hadi Sh243 milioni kwa sasa akisema nyongeza hiyo imetokana na faida kutoka kwa mali kama vile nyumba na biashara zingine za kibinafsi.

Wengine waliopigwa msasa Alhamisi ni Kithure Kindiki (Wizara ya Usalama wa Ndani), Deborah Barasa (Afya) Alice Wahome (Ardhi) na Julius Ogamba (Elimu).