Habari za Kitaifa

Sonko acheza kama yeye tena, asaidia mhanga wa ubakaji

Na BENSON MATHEKA December 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Mike Sonko, ametimiza ahadi yake ya kusaidia  mwanamke aliyenusurika ukatili wa ubakaji wa genge huko Laare, Meru, siku chache baada ya kutoa zawadi ya Sh300,000 kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa wahalifu.

Katika taarifa ya Ijumaa, Desemba 6, 2025, Sonko alifichua kuwa mwanamke huyo sasa yuko chini ya uangalizi kamili wa kimatibabu na ulinzi.

“Tulitoa ahadi na tunaitimiza. Mwanamke wa Meru aliyenusurika ubakaji wa kikatili sasa yuko chini ya matibabu kamili, ulinzi na msaada,” alisema Sonko.

Alisisitiza kuwa usalama wake utaendelea kulindwa akiongeza kuwa mkono wa sheria utawafikia wote waliohusika.

“Mwanamke kutoka Meru aliyepitia kikatili cha ubakaji wa kikundi sasa yuko chini ya huduma kamili za kiafya, ulinzi, na msaada. Hatakuwa peke yake, na hatatupwa. Kwa usalama wake, picha na  jina lake zitalindwa kikamilifu,” alisema Bw Sonko.

Huku  uchunguzi ukiendelea, washukiwa wengine sita wamekamatwa. “Hii sasa siyo kuhusu mwathiriwa mmoja au wawili — ni kuhusu haki, uwajibikaji na kutoa ujumbe usiotiliwa shaka kwamba yeyote anayewadhuru au kuwatisha binti, dada na mama zetu atashughulikiwa kwa nguvu zote za sheria.”

Washukiwa watatu walitiwa mbaroni siku ya tukio, na sasa jumla ya watu tisa wanazuiliwa huku ushahidi ukichambuliwa kabla ya kufikishwa mahakamani.

Tukio hilo lilitokea Desemba 1, 2025 wakati wa msafara  wa tohara katika mji wa Laare, Kaunti Ndogo ya Igembe Kaskazini. Polisi kutoka Kituo cha Laare walifika eneo la tukio baada ya kupokea taarifa za dharura, na kumkuta mwanamke huyo akiwa ameshtuka na nguo kuchanika, kisha wakampeleka Hospitali ya Nyambene kwa matibabu.

Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) ilianza mara moja msako, ikitumia teknolojia ya kisasa na kufanya operesheni maalum katika maeneo ya Irinde, Lubwa na Kiarama, ambako washukiwa sita walikamatwa.

Sonko alilaani kitendo hicho akisema mapambano haya yanahusu kurejesha haki na kuthibitisha kuwa ukatili dhidi ya wanawake hautavumiliwa.

“Tutawfuata kila mmoja wao. Tutasimama na mhasiriwa hadi haki itakapopatikana. Na hatutakoma kupigana hadi unyama huu ukomeshwe milele,” aliongeza.

Polisi wamesema msako dhidi ya washukiwa wengine unaendelea, huku Sonko akiahidi kuendelea kushirikiana nao kuhakikisha wahusika wote wanatiwa mbaroni.