Habari za Kitaifa

Sura mbili za Raila zazidi kupasua ODM

Na RUSHDIE OUDIA September 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WANACHAMA wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) wanaendelea kutoa hisia kinzani kuhusu uamuzi wa Raila Odinga kujiunga na serikali shirikishi, huku baadhi yao wakipinga kabisa hatua hiyo.

Mnamo Jumapili wanasiasa wanaoegemea chama hicho walipinga hadharani uamuzi wa Bw Odinga kufanya kazi na serikali ya Rais William Ruto huku wengine wakitoa tahadhari kuhusu ushirikiano huo.

Wanaopinga ukuruba wa kisiasa kati ya Rais Ruto na Bw Odinga walishikilia kuwa wataendelea kuikosoa serikali ya Kenya Kwanza inapokosea licha ya kwamba wanachama wao watano wanahudumu kama mawaziri katika serikali hiyo.

Chama cha ODM kimejipata katika hali ambapo kinataka kujihusisha na Wakenya ambao hawajaridhika na utawala wa Rais Ruto kwa upande mmoja na upande mwingine kikiendelea kuvuna manufaa ya kuwa serikalini.

Aidha, chama cha ODM kinataka kuendelea kushikilia uongozi wa mirengo ya wachache katika Bunge la Kitaifa na Seneti huku kikizuia juhudi za vyama tanzu katika Azimio  kuondoa wanachama wake katika uongozi wa kamati kuu za bunge zenye wajibu wa kuhakiki utendakazi wa serikali.

Mnamo Jumapili, wanasiasa wa ODM walikongamana nyumbani kwa Gavana wa Siaya James Orengo katika kijiji cha Nyawara, Masiro, eneo bunge la Ugenya kwa hafla ya ndoa mwanawe gavana huyo Michael Orengo na mkewe Samantha Luseno.

Wakati wa hafla hiyo Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alitumia methali ya Kiswahili kukionya chama hicho dhidi ya kuweka kando maono yake “kwa kitu kisichodumu”.

‘Usiache mbachao kwa msala upitao na usitupe ‘Big G’ kwa karanga za kuonjeshwa,’ Seneta huyo wa Nairobi akasema.

“Kwa Samantha na Michael, mkijitolea kwa safari muwe mzingatie maono yenu maishani. Mike ukiona umerushiwa njugu nne kama zile ambazo walirushia ODM, usimteme Samantha,” akasema Bw Sifuna.

Akaongeza: “Sharti kujifunze kutokana na yale yanayomkumba Rigathi Gachagua ambaye aliiingia katika muungano bila mashahidi au mkataba. Sharti tusalie thabiti ndani ya ODM.”

Naye Mbunge Mwakilishi wa Kisumu Ruth Odinga, dadake Raila alisema wakati huu ODM iko katika ndoa ya ‘njoo tuishi’ na Rais Ruto ndoa ambayo mustakabali wake haujulikani.

“Ruto aliwachukua watu watano pekee lakini kilicho muhimu ni kwamba wengi wetu katika ODM hatuko katika ndoa hiyo. Tumeteseka katika chama hicho na hatuwezi kujiunga na chama kidogo kama UDA. Tusihadaiwe na zawadi ndogo kama ‘popcorn’ tunayopewa,” akasema Bi Odinga.

Kwa upande wake Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang’ aliwataka wabunge na maseneta wa ODM kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kuhakiki utendakazi wa serikali ya Dkt Ruto.

“Kama chama tunapaswa kuhakikisha kuwa tunazingatia wajibu wetu jinsi Raila amekuwa akifanya katika kuhakikisha kuwa nchi hii imekombolewa kutoka kwa utawala wa udikteta na ukabila. Tusipotoshwe. Tuendelea kuongea lugha ya wananchi,” akasema.

Mwenzake wa Nyamira Okong’o Omogeni alisema alijiunga na ODM kwa sababu alimpenda na kumheshimu Bw Odinga.

“Hatukatai kwamba Bw Odinga alikuwa akimwokoa Rais Ruto, na tunaamini kuwa hataleta urais magharibi mwa Kenya tulivyotaka. Sharti tuzingatie lengo hilo,” akasema Bw Omogeni.

Lakini Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo alielezea matumaini kuwa ushirikiano kati ya Rais Ruto na Bw Odinga utarasimishwa “hivi karibuni.”