Trump atandika Kenya na ushuru
KENYA imepata pigo katika biashara yake na Amerika baada ya Rais Donald Trump kutia saini agizo linaloweka ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa zote kutoka Kenya zinazoingizwa nchini humo.
Hatua hiyo inaenda kinyume na Sheria ya AGOA, iliyopitishwa mwaka wa 2000, inayoruhusu mataifa 32 ya Afrika ikiwemo Kenya kuuza bidhaa nchini Amerika bila kutozwa ushuru.
Muda wa utekelezaji wa sheria hiyo unapasa kukamilika mnamo Septemba 22, 2025, baada ya kuongezwa mara kadhaa tangu 2015.
Chini ya AGOA, Kenya huuza bidhaa za nguo pamoja na zile za kilimo kama vile kahawa, majani chai, macadamia na mboga na matunda, nchini Amerika.
Katibu wa Masuala ya Kigeni wa Kenya, Korir Sing’oei, alipuuza uzito wa athari za ushuru huo mpya, akibainisha kuwa Kenya bado ina viwango vya chini zaidi vya ushuru na imewekwa katika kundi moja na Uingereza, Misri, Morocco, Uganda, Tanzania, na Ethiopia.
Bw Sing’oei alisema kuwa Kenya itashinikiza msamaha wa ushuru huo lakini akasisitiza kuwa hautaathiri nchi mara moja.
Alieleza kuwa Sheria ya AGOA inaruhusu nchi za Afrika kuendelea kuuza bidhaa zao nchini Amerika bila ushuru hadi makubaliano hayo yatakapomalizika mwezi Septemba.
“Kwa kuwa AGOA ni mfumo wa kisheria wa Bunge la Amerika kwa upatikanaji wa soko la Amerika kwa wauzaji wa Afrika, mtazamo wetu ni kwamba hadi sheria hii itakapomalizika mwishoni mwa Septemba 2025, au isipofutwa mapema na Bunge la Amerika, ushuru mpya uliowekwa na Rais Trump hautaanza kutekelezwa mara moja.”
Kenya imekuwa ikitoza ushuru wa asimilia 10 kwa bidhaa kutoka Amerika zinazoingizwa nchini.
Sasa kufuatia ushuru uliowekwa na Trump Jumatano, biashara ya thamani ya Sh109.7 bilioni kati ya Kenya na Amerika itaathirika pakubwa kwani kiasi cha bidhaa zitakazouzwa nchini humo kitapungua.
Wadadisi wanasema kuwa hali hii itachangia kupungua kwa mapato kwa kampuni za humu nchini zinazotegemea soko la Amerika na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hizo kufutwa kazi.
“Kufuatia tangazo hilo la Trump, bila shaka kampuni za kutengeneza nguo za kuuzwa nje (EPZ) kama vile zilizoko eneo la Athi River zitaathirika kimapato na kuamua kuanza kupunguza waajiri. Hali hii itachangia ongezeko la kero la ukosefu wa ajira nchini,” anasema Barasa Nyukuri ambaye ni mtaalam katika masuala ya uchumi
Kulingana na takwimu kutoka Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS), kufikia Desemba 2024, jumla ya Wakenya 75, 598 walikuwa wameajiriwa moja kwa moja katika EPZs nchini.
Akitoa tangazo kuhusu agizo hilo Jumatano usiku, katika Ikulu ya White House, Rais Trump alishikilia kuwa lengo la ushuru huo ni kulinda masilahi ya Amerika katika biashara kati yake na mataifa yote ya ulimwenguni.
Alieleza kuwa hiyo ni sehemu ya mpango wa kubadilishwa kwa sera ya kibiashara ya Amerika, akitaja siku kama “Siku ya Ukombozi”.
“Agizo hilo linaashiria mwanzo wa uhuru wetu kiuchumi,” Trump akasema akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kujenga uchumi wa Amerika na “na kuzuia kunyanyaswa kwetu na mataifa mengine.”
Kenya ni miongoni mwa mataifa yaliyotajwa kwenye agizo la Trump kama miongoni mwa mataifa lengwa kwani hutoza ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa kutoka Amerika.
“Tutatoza kiwango kama hicho cha ushuru kwa bidhaa zote zinazoingizwa Amerika. Tunaendelea kuirejeshea Amerika hadhi yake,” Trump akaeleza.
Kando na Kenya, mataifa mengine katika Ukanda wa Afrika Mashariki yatakayoathirika na agizo la Trump ni Tanzania, Uganda, Rwanda na Sudan Kusini.
Wakati huo huo, Kenya imepata pigo jingine baada Wizara ya Serikali kuhusu Ufanisi (DOGE) kufutilia mbali kandarasi za Amerika nchini Kenya za thamani ya zaidi ya Sh10 bilioni.
Kwenye taarifa Alhamisi, Juni 3, 2025, wizara hiyo inayoongozwa na bwanyenye Elon Musk, ilisema hatua hiyo inaendana na wajibu wake kufutulia mbali kandarasi “zisizo na faida”.
“Asasi zilifutilia mbali kandarasi 47 zisizo na faida ikiwemo ile ya thamani ya Dola 3.4 milioni (Sh439 milioni) za washauri kuhusu masuala ya safari za angani Kenya,” ikasema taarifa hiyo.
Februari 2025, DOGE ilifutilia mbali msaada wa thamani ya Dola 79 milioni (Sh10.2 bilioni) kwa Idara ya Elimu ya msingi nchini Kenya.
Aidha, wizara hiyo ilikata misaada mingi iliyopangiwa kuelekezwa katika mataifa yanayoendelea katika Bara la Afrika na Amerika Kusini.
Kufutiliwa kwa kandarasi hizi kunajiri baada ya Rais Trump kukatiza ufadhili kwa miradi na mipango kadha inayoendeshwa na Shirika la Amerika kuhusu Maendeleo ya Kimataifa (USAID) nchini Kenya.
Kulingana na ripoti moja ya Amerika, jumla ya miradi 72 kati ya 83 iliyokuwa ikiendeshwa na USAID ilizimwa, ikisalia miradi 11 iliyoko katika sekta ya afya.