TSC yaanza kunoa walimu kwa maandalizi ya masomo ya Gredi 9
TUME ya Kuwaajiri Walimu (TSC) ikishirikiana na Wizara ya Elimu imeanza kufunza walimu wakuu wa shule za sekondari namna ya kusaidia wanafunzi wa Gredi ya Tisa wanaotarajiwa kujiunga na Sekondari Msingi kuchagua taaluma wanazoazimia kufanya.
Aidha, walimu hao watakuwa na jukumu kubwa la kuwasaidia wanafunzi hao kuchagua mkondo wao wa maisha wakiwa shuleni.
Mwaka ujao, 2026, zaidi ya wanafunzi 1.2 milioni watajiunga na shule za upili kulingana na taaluma wanaotazamia kufanya.
Kwa mfano, shule za kitaifa zinatarajiwa kuchukua mikondo mitatu, ikiwemo spoti na sayansi.
Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC, Bi Nancy Macharia, alisema mafunzo hayo yatasaidia walimu wakuu kusaidia wanafunzi kuchagua taaluma zao.
“Watachagua taaluma kulingana na uwezo wao wa kimasomo na matamanio yao. Lakini tunawapa haya mafunzo kuhakikisha mnawasaidia kuchukua mkondo wao wa maisha,” alisema Bi Macharia.
Bi Macharia aliwakilishwa na mkurugenzi wa walimu Bi Antonina Lentoijoni kwenye kongamano la zaidi ya walimu 1000 wa shule za upili kutoka kaunti saba ikiwemo Muranga, Kiambu, Nyandarua, Nakuru, Machakos, Makueni, Tharaka Nithi na Laikipia.
Kote nchini TSC na Wizara ya Elimu zinawapa walimu 7,000 mafunzo hayo sehemu kadhaa.
Bi Lentoijoni alisema warsha hiyo imejiri wakati mwafaka Kenya inapopitia mageuzi ya elimu kutoka mfumo wa 8-4-4 hadi ule wa CBC unaonuia kubadilisha maisha ya wanafunzi nchini.
Aliwapongeza walimu wakuu kutoka Murang’a kupitia chama chao cha KESSHA kwa kuandaa hafla hiyo.
“Kenya imepiga hatua kubwa sana katika sekta ya elimu, mwakani (2026) tutashuhudia mageuzi kabambe wakati watoto wetu watakapojiunga na shule za upili yaani Gredi ya 10 inayolenga kukuza talanta zao,” alisema Bi Macharia.