Habari za Kitaifa

Tuju sasa aripoti Koome kwa EACC

Na HAPPINESS LOLPISIA March 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA Waziri, Raphael Tuju, Jumanne, Machi 25, 2025 aliwasilisha malalamishi kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuhusu madai ya ukiukaji wa maadili na uwezekano wa ufisadi ndani ya Mahakama ya Juu Zaidi ya Kenya.

Bw Tuju alisisitiza kuwa hakuenda katika ofisi za EACC kuhojiwa kwa madai ya ufisadi.

“Hii ni mara yangu ya kwanza kufika EACC. Sina masuala yoyote ya ufisadi,” alisema.

Alidai baadhi ya majaji wamekuwa wakizungumzia hadharani kesi zao kinyume na maadili ya mahakama.

Bw Tuju amewasilisha ombi katika Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) akitaka majaji wote saba wa Mahakama ya ya Juu Zaidi waondolewe kwa madai ya ukiukaji wa maadili. Alieleza kuwa alikuwa wameandika barua kwa Jaji Mkuu (CJ) Martha Koome na anasubiri majibu.

Katika makao makuu ya EACC alipokelewa na Mwenyekiti wa EACC, Askofu Dkt David Oginde, na akawasilisha ripoti faraghani kwa uchunguzi zaidi.

Moja ya malalamishi makuu ni madai kuwa Mahakama ya Juu Zaidi imezuia JSC kutekeleza majukumu yake huku majaji wakiwasilisha kesi zao mbele ya mahakama za chini.

Tuju alikosoa majaji kwa upendeleo katika mzozo wa deni la Sh1.2 bilioni kati yake na Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) na kutumia lugha kali katika kesi ya urais wa 2022.

Hatua yake imezua mjadala mkali, huku wengine wakimuunga mkono kwa kudai uwajibikaji wa mahakama, ilhali wengine wakichukulia kama jaribio la kudhoofisha uhuru wa mahakama.