Habari za Kitaifa

Ujanja wa magavana wenye mikosi kuepuka kubanduliwa kama Mwangaza

Na MOSES NYAMORI August 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KARIBU magavana 10 wamelazimika kutumia ujanja wa kisiasa kuponea masaibu sawa na yanayomkumba mwenzao wa Meru, Kawira Mwangaza.

Bi Mwangaza alipata afueni ya muda Jumatano, Agosti 21, 2024 baada ya kutimuliwa afisini Jumanne (Agosti 20, 2024) na maseneta walioidhinisha hoja iliyopitishwa na madiwani wa Meru.

Hoja hiyo ilionekana kuchochewa na uhasama wa kisiasa kati ya gavana huyo, aliyechaguliwa kwa tiketi huru, na madiwani hao na wanasiasa wengine wa kaunti hiyo.

Lakini mbinu za kisiasa zinazotumiwa na magavana tisa, ambao walichaguliwa kwa tiketi huru au vyama visivyo na ushawishi mkubwa katika kaunti zao zimeonekana kuwanusuru.

Wao ni pamoja na Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha UDA katika ngome hii ya Azimio, Andrew Mwadime (Taita Taveta, tiketi huru), Jeremiah Lomorukai (Turkana, ODM), George Natembeya (Trans Nzoia, DAP-K), Simon Kachapin (Pokot Magharibi, UDA), Jonathan Lati Lelelit (Samburu, UDA), Joseph Lenku (Kajiado, ODM), Abdi Guyo (Isiolo, Jubilee) na gavana wa Lamu Issa Timamy aliyedhaminiwa na chama cha Amani Nationa Congress (ANC).

Magavana hawa, kwa mfano, wameamua kimakusudi kukidhia matakwa, na masilahi ya kisiasa ya madiwani na viongozi wa vyama au miungano ya walio wengi katika kaunti wanazoongoza.

Mbinu hii, ambayo Bi Mwangaza alichelea kuitumia Meru, imewasaidia kuendelea na uongozi bila usumbufu.

Katika kaunti ya Nairobi, Bw Sakaja aliamua kuwateua wandani wa kiongozi wa ODM Raila Odinga katika serikali yake ili kupata uungwaji mkono kutoka kwa Azimio la Umoja-One Kenya yenye idadi kubwa ya madiwani katika bunge la kaunti hiyo.

Katika kaunti ya Nairobi, Gavana Sakaja ndiye kiongozi wa kipekee aliyechaguliwa kwa tiketi ya UDA katika ngazi ya kaunti.

UDA ilipoteza nafasi za Seneta na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake ambazo zilitwaliwa na chama cha ODM.

Na kati ya maeneo bunge 17, Azimio ilishinda viti 13 huku UDA ikishinda viti vinne pekee.

“Katika Bunge la Kaunti ya Nairobi, kati ya viti 85, tulipata viti 35 pekee. Ukijipata katika hali kama hiyo, utahitajika kuzinduka na kufanya kazi na wanasiasa kutoka vyama vyote,” Bw Sakaja akasema.

“Hii ina maana unafungua milango ya mazungumzo. Unashirikisha viongozi waliochaguliwa na viongozi wa vyama vyao,” akaongeza.

Gavana Sakaja alisema mwanzoni, alikumbwa na matatizo na madiwani wa UDA, lakini alipoanza kufanya kazi na upande wa Azimio wote waligundua kuna ubora wa kufanya kazi kwa ushirikiano.

“Mara kadhaa, nimekuwa nikikutana na kiongozi wa ODM Raila Odinga hata kabla ya kukutana na Rais William Ruto kujadili masuala yanayohusiana na shughuli za kaunti ya Nairobi,” akaeleza, akiongeza kuwa siasa haipasi kuleta uadui.

Naibu Gavana wa Machakos, Francis Mwangangi aliambia Taifa Dijitali kwamba, baadhi ya magavana hujipata kwenye shida kwa sababu wao hujaribu kufanya kazi kivyao.

Alishauri kwamba njia ya pekee ya kuponea hujuma za kisiasa ni kuwashirikisha wanasiasa wote katika mipango ya kaunti.

“Kiongozi yeyote aliyechaguliwa katika ngazi yoyote anafaa kuelewa kuwa, kuna wadau wengi ambao anafaa kushauriana nao aweze kujiendeleza kisiasa,” akasema Bw Mwangangi.

“Ikiwa hauna moyo wa kufanya kazi pamoja, bila shaka utajipata ukikosana na wanasiasa katika kaunti yako. Aidha, unafaa kufuatilia kwa makini hali ya siasa katika ngazi za mashinani na kitaifa,” akaongeza.

Katika kaunti ya Kajiado, Gavana Lenku aliyechaguliwa kwa tiketi ya ODM amekumbatia mbinu alizokumbatia Bw Sakaja, kwa kupalilia uhusiano mzuri na madiwani wa UDA, walio wengi.

Hali sawa na hiyo inashuhudiwa katika kaunti ya Isiolo ambapo Gavana Guyo aliyechaguliwa kwa tiketi ya Jubilee amekumbatia madiwani wa UDA.

Akitambua kwamba, anazingirwa na madiwani wengi wa chama pinzani cha Ford Kenya cha Spika Moses Wetang’ula, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya wa chama cha DAP- Kenya ameamua kujenga umaarufu mashinani na kujivumisha kupitia vuguvugu lake la Tawe.

Hii imemfanya kuwa maarufu na kuwafunika wawakilishi wadi wanaoonekana kutomsumbua.