Umekumbana na noti mpya ya Sh1, 000?
IWAPO umekuwa makini kutazama hela zako kila unapozitumia katika shughuli mbalimbali zinazohusu pesa, basi umegundua kuna noti mpya za Sh1, 000.
Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Fedha ilielezwa Jumatano, Agosti 21, 2024 kwamba Benki Kuu ya Kenya (CBK), ilitoa taarifa ikiarifu umma kuwa imetoa noti mpya za Sh1, 000 ambazo tayari zimeanza kutumika na umma. Zilizosalia zinakuja hivi karibuni.
Mkuu wa CBK, Kamau Thugge, alieleza Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Molo, Kuria Kimani kwamba Kenya imetia saini kandarasi ya Sh14.2 bilioni na kampuni ya Ujerumani ya kuchapisha pesa, Giesecke & Devrient Currency Technologies GmbH (G+D).
Noti zinazotumika kwa sasa zilichapishwa 2019 na shirika la De La Rue Kenya EPZ, lililofunga kiwanda chake katika jiji kuu la Nairobi, Januari 2023 baada ya kandarasi yake kukamilika.
Akitetea uamuzi wa kuchapisha noti nyingine mpya katika kipindi cha miaka mitano tu, Dkt Thugge alisema hatua hiyo iliafikiwa baada ya kugundua taifa linakabiliwa na tishio la kuishiwa na noti.
“Hali ya kuishiwa na noti ina hatari kubwa kiuchumi na kitaifa. Kulikuwa na tishio la kuishiwa na noti za Sh1, 000,” alifafanua Mkuu huyo wa CBK.
Akijibu kuhusu Mbunge wa Eldas, Adan Keynan, kuhusu ni kwa nini De La Rue ilifunganya virago na kuondoka huku ikiwaacha mamia ya Wakenya bila kazi, Dkt Thugge alifafanua kuwa, “De La Rue ilifunga kwa hiari yake. Ilifanya uamuzi wa kuondoka.”
Alisema kandarasi hii mpya, kando na kuzingatia sheria za ununuzi, ilikuwa na thamani ya kifedha ikiinganishwa na iliyotangulia.
“Gharama ya noti za benki ilikuwa Sh14.2 bilioni kwa kutumia thamani ya sarafu wakati wa kutia saini mkataba. Kandarasi ya noti zilizochapishwa 2019 iligharimu Sh14.5 bilioni.”
Kandarasi hiyo mpya inakusudiwa kuchapisha noti 460 milioni za Sh50, noti 690 milioni za Sh100, noti 260 milioni za Sh200, noti 170 milioni za Sh500, na noti 460 milioni za Sh1, 000, alieleza Mkurugenzi wa Sarafu CBK, Paul Wanyeki.
Alisema Wakenya huwa makini zaidi wanaposhika noti ya Sh1, 000 ikilinganishwa na noti za Sh50, Sh100, na Sh200 ambazo nyingi zimechakaa hivyo haja ya kuchapisha noti mpya.
“Katika mataifa kama vile Amerika au Uingereza, unapata kila mtu anahifadhi noti katika mfuko zikiwa zimepangwa vyema. Lakini wengi wetu, hasa sokoni, unapata noti zimekunjwa na kusindiliwa mfukoni. Kwa kufanya hivyo, nyuzi za noti huwa dhaifu, noti zinakuwa chafu. Zinaporejea kwetu, zinakuja katika hali ambayo hatuwezi kuziachilia kwa raia,” alifafanua Bw Wanyeki.
“Tunaishia kuziondoa na kuleta nyingine. Hayo hutokea hasa kwa Sh50, Sh100, na Sh200. Kwa Sh1, 000, watu huwa makini sana. Ni nadra kupata watu na noti ya Sh1, 000, huwa inahifadhiwa vizuri sana.”
“Hakuna jibu moja kuhusu ni muda gani noti zinapaswa kudumu kabla ya kubadilishwa. Zinaweza kudumu hata kwa miaka mitatu, mitano au hata siku moja kulingana na zinavyohifadhiwa. Noti nyingi tunazoondoa, baadhi hata huwa zimechorwa, zingine zimeraruka, zimekunjwa na hata kukunjana.”