Habari za Kitaifa

UN yalaani mauaji ya mwanariadha Rebecca Cheptegei

Na FRANCIS MUREITHI September 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Afya ya Uzazi (UNFPA) Natalia Kanem amelaani mauaji ya kikatili ya mwanariadha shujaa wa Olimpiki Rebecca Cheptegei.

Mwendazake aliuawa na mpenziwe wa zamani ambaye ni Mkenya kutokana na kile kilichotajwa kama mzozo wa ardhi.

“Tunaomboleza kifo chake na kutuma rambirambi kwa familia na jamaa zake. Kifo cha Rebecca kinaonyesha dhuluma ambazo wanawake kote ulimwenguni hutendewa, haswa na wale wale wanaowaamini zaidi,” akasema Dkt Kanem kwenye taarifa.

Rebecca, 33, alikuwa mwanariadha wa mbio za masafa marefu na aliyeshikilia rekodi ya kitaifa katika mbio za marathon nchini Uganda. Aidha, alishikilia mshindi wa dunia katika mbio za milima.

Mwanariadha huyo aliaga dunia mnamo Septemba 5 katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH), Eldoret, baada ya kuteketezwa ndani ya nyumba na Dickson Ndiema eneo la Trans Nzoia.

Shirika la Kutetea Haki, Amnesty International, tawi la Kenya, limelaani mauaji hayo likisema “ipo haja ya visa vya mauaji ya wanawake kudhibitiwa nchini.”

Kulingana na UNFPA, zaidi ya nusu ya visa vya mauaji ya wanawake hutekelezwa na wapenzi wao au watu wengine wa familia.

Mwanamke huuawa na mtu wa familia yake ndani ya kila dakika 11, kulingana na takwimu za ulimwengu kuhusu mauaji ya wanawake zilizotolewa 2023.

Hata hivyo, inabashiriwa kuwa huenda idadi halisi ya visa hivyo ikawa juu.

Inakadiriwa kuwa mnamo 2022, wanawake na wasichana 89,000 waliuawa kimakusudi ulimwenguni.

Dkt Kanem alisema dhuluma za kijinsia ni miongoni mwa visa vikuu vya ukiukaji wa haki ambavyo havijali mipaka ya kijamii, kiuchumi au kitaifa.

“Dhuluma za kijinsia huathiri afya, heshima, usalama na uhuru wa waathiriwa. Hufichwa kutokana imani za kitamaduni na nyakati fulani huchukuliwa kama jambo la kawaida katika mahusiano,” akasema mkurugenzi huyo wa UNFPA.

Dkt Kanem alitoa wito kwa hatua za pamoja zichukuliwe ulimwenguni kukinga wanawake na wasichana kutokana na dhuluma hizo.

“Wanahitaji amani katika nyumba zao na jamii. Serikali zinahitaji kutoa usaidizi bora kwa wahasiriwa, kwa kuhakikisha wanapata makazi mbadala, huduma za afya na uwakilishi wa kisheria kuwakinga dhidi ya wadhalimu hao,” akaongeza.

“Wakati umetimu kwa wanaume na wavulana kuachana na dhana potovu zinazofanya dhuluma hizo kuwa jambo la kawaida. Tunapaswa kuchunguza chimbuko halisi la dhuluma za kijinsia zikiwemo mila na tamaduni na hisia kwamba miili ya wanawake ni mali ya wanaume,” Dkt Kanem akaeleza.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga