Habari za Kitaifa

Ushuru wa AFA kupandisha bei ya mchele na unga wa ngano

Na ANTONY KITIMO, CHARLES WASONGA August 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

BEI ya mchele na unga wa ngano itaanza kupanda mwezi huu baada ya serikali kuanza kutoza ushuru wa asilimia 2 kwa  thamani ya nafaka inayoagizwa kutoka nje.

Kuanzia Agosti 12, 2024 aina zote za nafaka na maharagwe yanayoingizwa nchini zilianza kutozwa ushuru huo mpya ulioanzishwa na Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA).

Wafanyabiashara wanapinga ushuru huo wakisema utaongeza gharama kwa kuendesha biashara zao.

Kando na ushuru wa asilimia mbili kwa thamani ya nafaka inayoingizwa nchini AFA pia imeanzisha ushuru wa kima cha asilimia 0.3 ya thamani ya nafasi inayouzwa nje ya Kenya.

AFA pia imeanzisha ushuru wa asimilia 2 ya thamani ya mazao ya maharagwe na kunde yanayoingizwa nchini kutoka ng’ambo.

Viazi kuwa ghali

Kwa upande mwingine, viazi, mihogo na viazi vikuu kuu vinavyoingizwa nchini kutoka nje vitatozwa ushuru wa asilimia moja ya thamani yake.

Na wale wanaouza mazao hayo nje ya Kenya watatozwa ushuru wa kima cha asilimia 0.3 ya thamani ya bidhaa hizo.

AFA ilitoa notisi yenye maagizo hayo kwa mujibu wa hitaji la kanuni nambari 37 ya Kanuni kuhusu Mazao ya Chakula ya 2019 ambayo ilitarajiwa kutekelezwa Julai 1, 2024 lakini tarehe ya utekelezaji wake ikasongezwa hadi Agosti 12, mwaka huu.

Kulingana na AFA, ushuru husika zitalipwa moja kwa moja kwa maajenti wake katika vituo vya kuingia na kuondoka Kenya.

Kuanzishwa kwa ushuru kwa bidhaa za vyakula zinazoingizwa nchini kutasaidia wakulima wa mazao ya chakula humu nchini kushindani vizuri na mazao yanayoingizwa nchini kutoka nje.

Wafanyabiashara watakaofeli kulipa ushuru huo watatozwa faini ya asilimia 25 ya kiasi cha ushuru wanachodaiwa katika mwezi ambao hawakulipa.

Kwa mujibu wa agizo hilo la AFA, wafanyabiashara wa nafaka na maharagwe watalipa Sh20,000 zaidi ya matozo ya kawaida kwa lori la mahindi na Sh50,000 zaidi, ya matozo ya kawaida,  kwa lori moja la mchele.

Wafanyabiashara hao wamekuwa wakilipa matozo hayo kwa asasi mbalimbali za serikali kama vile Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA), Shirika la Kuchunguza Afya ya Mimea (Kephis) na Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa (Kebs).

Kando na ushuru wa AFA, wafanyabiashara wanaoingiza mazao ya nafaka na maharagwe nchini watahitajika kulipa Sh3,000 kwa leseni ya AFA, ada ya Sh600 kwa leseni ya uagizaji na Sh7,500 kama ada ya ukaguzi kwa Kephis, Sh1,100 kama ada ya usafi wa bandari, Sh1, 100 kama ada ya “biosafety” na Sh7,200 kwa Kebs kama ada ya ukaguzi wa viwango vya  unyevu na viwango vya sumu ya aflatoxin katika mazao hayo ya chakula.

Afisa Mkuu wa Baraza la Usafirishaji Bidhaa kwa Meli Afrika Mashariki Agayo Ogambi alisema ada hizo zinaduma ukuaji wa biashara na zitaongeza mzigo kwa wakulima na waagizaji kutoka nje na wauzaji wa mazao ya chakula ambao tayari wanalipa ada nyingi za kibiashara kwa serikali ya Kenya.