Habari za Kitaifa

Vijana hawataki mazungumzo na Ruto wanataka haki, Kalonzo akosoa Raila

Na PIUS MAUNDU July 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, amepinga wito wa kiongozi wa ODM Raila Odinga wa kuandaa mazungumzo ya kitaifa kati ya vizazi mbalimbali, kufuatia maandamano ya vijana dhidi ya serikali.

Akizungumza Alhamisi katika hafla ya kufungua hospitali ya jamii mjini Kiongwani, Kaunti ya Makueni, Bw Musyoka alisema kuwa ni wajibu wa kikatiba wa Rais William Ruto kushughulikia malalamishi ya vijana wanaoendelea na maandamano barabarani na mitandaoni.

“Raila anasema tuzungumze na Ruto. Tunajiuliza, mazungumzo hayo yatafaidi nani? Hawa watoto hawahitaji mazungumzo – wanahitaji haki. Wanataka elimu ya msingi na sekondari bila malipo kama alivyofanya marehemu Rais Mwai Kibaki,” alisema Bw Musyoka.

“Wanataka kujiunga na vyuo vikuu kupitia mfumo wa ufadhili unaoeleweka, si huu wa sasa wa mkanganyiko,” aliongeza.

Bw Musyoka alikuwa ameandamana na Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Makueni, Rose Museo, Spika wa Bunge la Kaunti Douglas Mbilu, Naibu Gavana Lucy Mulili na Mbunge wa Kilome Thadeus Nzambia.

Wote walitumia jukwaa hilo kumshutumu Rais Ruto kwa kile walichokitaja kama uongozi mbaya, ukosefu wa uwajibikaji na ufisadi. Pia walitoa wito kwa Wakenya kuukataa mrengo wa Kenya Kwanza kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Bw Musyoka kuzungumzia kwa kina pendekezo la Bw Odinga kuhusu mazungumzo ya kitaifa ambayo yamekuwa yakitolewa kama suluhu kwa mgogoro kati ya serikali na vijana.

Kwa mujibu wa Bw Odinga, kikao hicho cha mazungumzo kitawahusisha viongozi mashuhuri na wawakilishi wa vijana kutoka maeneo mbalimbali ya nchi ili kuhakikisha uwakilishi wa kila upande.

Aidha, alisema mazungumzo hayo yatatoa fursa ya kujadili masuala muhimu kama vile ukosefu wa ajira kwa vijana, uwajibikaji wa serikali, vita dhidi ya ufisadi, na mageuzi ya polisi.

“Ninapendekeza kwamba jukwaa hilo la kitaifa liandae mkakati wa kina na wa kudumu wa kushughulikia tatizo la ajira kwa vijana pamoja na upanuzi wa fursa katika sekta rasmi na isiyo rasmi,” alisema Bw Odinga wiki iliyopita.

Hata hivyo, Kalonzo alikosoa vikali wazo hilo, akisisitiza kuwa suluhu ya matatizo ya vijana haiko kwenye mazungumzo bali utekelezaji wa haki na sheria.

Katika hotuba yake, Bi Rose Museo alitoa wito kwa vijana kuacha maandamano na badala yake wajitokeze kujiandikisha kama wapiga kura kwa uchaguzi ujao.

“Tumechoka kuwasindikiza watoto wetu makaburini. Wanauliwa na wale wanaopaswa kuwalinda. Njia sahihi ya kumuondoa Ruto ni kwa kura, si maandamano,” alisema Bi Museo.