Habari za Kitaifa

Viongozi wa kidini wapinga mpango wa kurefusha muhula wa Ruto

Na EVANS JAOLA, LABAAN SHABAAN October 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

BAADHI ya viongozi wa kidini kutoka eneo la magharibi, wamepinga Mswada wa Seneta wa Nandi Samson Cherargei unaolenga kuongeza muhula wa kuhudumu wa rais na maafisa wengine waliochaguliwa.

Chama cha Viongozi wa Makanisa Kenya kimesema hakiungi mkono pendekezo hilo katika Mswada wa Sheria ya Kurekebisha Katiba ya 2024, linalolenga kuongeza muhula wa rais kutoka miaka mitano hadi saba, na mabadiliko sawa na hayo kwa magavana na Wabunge.

Mwenyekiti wa Kitaifa Askofu Hudson Ndeda alisema miaka mitano inatosha kwa muhula wa rais na viongozi waliochaguliwa.

‘Hatuungi mkono mipango ya kuongeza muhula wa kuhudumu wa viongozi waliochaguliwa, kwani tunaamini miaka mitano inatosha kwa viongozi kutimiza majukumu yao,’ Askofu Ndeda alisema.

Alisisitiza kuwa ni vyema kuangazia masuala muhimu yanayowakabili Wakenya, kama vile kupanda kwa gharama ya maisha badala ya kuongeza muda wa viongozi kuhudumu.

Haya yanajiri huku viongozi wa kidini ambao walimuunga mkono Dkt Ruto kuwa rais wa tano wa jamhuri ya Kenya wakianza kujitenga na sera za serikali.

Baraza la Kitaifa la Makanisa la Kenya limekuwa likishutumu utawala wa Kenya Kwanza kwa kuvunja ahadi za kabla ya uchaguzi.

Viongozi hawa wamekiri kwamba utawala wa sasa unaungwa mkono na kanisa, lakini washiriki hawakufurahishwa na ongezeko la kodi pamoja na sera zingine dhalimu zinazohujumu biashara.

Makasisi wanamtaka Rais Ruto kubadili sera zake wakisema kuwa zinasababisha maumivu na vilio miongoni mwa Wakenya wakimkumbusha kuwa Wakenya hawakumchagua awahangaishe na msururu wa ushuru.