Viongozi wa ODM wataka Gachagua atengwe zaidi
SENETA wa Siaya Dkt Oburu Oginga na mwenzake wa Homa Bay Moses Kajwang’ wametaka utawala wa Kenya Kwanza umtenge aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kabisa wakiahidi kuhakikisha upande ambao anauegemea haushindi uchaguzi mkuu ujao.
Viongozi hao wawili wamesema Bw Gachagua alionyesha ukabila mtupu kwa muda wa miaka miwili alipokuwa makamu wa rais kwa kutenga maeneo mengine na kutaka Mlima Kenya unufaike pekee.
“Wakati wa maandamano ya Gen Z, sote tulisema lazima Ruto aende lakini angeenda, Bw Gachagua angechukua mamlaka ilhali alikuwa akipangia tu mgao wa watu kutoka eneo lake,” akasema Dkt Oginga.
“Watu wetu na ngome nyinginezo za Raila zingetengwa zaidi iwapo Bw Gachagua ndiye angekuwa akiongoza taifa kwa sasa,” akaongeza Dkt Oginga.
Naye Seneta Kajwang’ alimrejelea aliyekuwa naibu rais kama mwanasiasa asiyeweza kuona mbali pamoja na washirika wake wa kisiasa.
Kwa mujibu wa Bw Kajwang’, Bw Gachagua hataenda mbali na chama chake kipya cha DCP ikizingatiwa sheria ilifuatwa katika kuondolewa kwake mamlakani.
“Kama una akili timamu, unamfuataje mtu ambaye hana mustakabali wa kisiasa. Nawasikitia watu kama Justin Muturi ambao wanamfuata Bw Gachagua aliyeondolewa mamlakani na hawezi kugombea kiti chochote,” akasema Bw Kajwang’.
Wawili hao pamoja na wanasiasa wengine wa ODM walikuwa wakizungumza katika mazishi moja eneo la Wiga viungani mwa mji wa Homa Bay mnamo Ijumaa.
Wakati wa hafla hiyo, walishikilia kwamba ODM itaendelea kushirikiana na utawala wa Rais William Ruto ili inufaikie kwa miradi ya maendeleo, wakisema ukuruba huo huenda ukaendelea hata baada ya 2027.
“Kuna mwanya wa watu wetu kuonja kitu serikalini ndipo hata sisi tunufaikie mgao ambao tulikuwa tunanyimwa. Hata sisi ni walipaushuru,” akasema Dkt Oginga.
Seneta huyo ambaye ni Kakake Kinara wa Upinzani Raila Odinga alisema ushirikiano wa ODM na UDA utaendelea hadi 2027 na Bw Gachagua hatakuwa na nafasi ya kuvuruga uhusiano huo hata akitumia chama chake kipya cha DCP.
“Tulimwaambia Bw Gachagua kuwa Raila ndiye alikuwa kiongozi mzuri na angegawa rasilimali za nchi kwa usawa. Sasa tunaunga Ruto ambaye alikuwa mwaniaji wao na wanajitokeza eti tufanye nao ndio waunge Raila 2027,” akasema.
Alisisitiza kuwa hakuna hakikisho lolote kuwa Bw Gachagua na mrengo wake wa kisiasa watamuunga Raila 2027.
“Wasubiri tuwafanyie watu wetu kazi na wakitaka tushirikiane watutafute mnamo 2027 na watueleze kile kilichoko mezani kisha tujadiliane na tuamue. Kwa sasa tupo katika Serikali Jumuishi na hatujutii hatua yetu,” akasema.
Wabunge wengine ambao walihudhuria mazishi hayo ni Samuel Atandi (Alego Usonga), Aduma Owuor (Nyakach) na Peter Kaluma (Homa Bay Mjini).
Wote waliunga Serikali Jumuishi na kuwataka mawaziri wa ODM wahakikishe eneo hilo linanufaika kwa miradi ya maendeleo.