Vitabu 7 vya Kiswahili kushindania tuzo za Jomo Kenyatta Prize 2024
VITABU saba vya Kiswahili ni kati ya vitabu 13 vilivyoorodheshwa kushindania tuzo mbalimbali kwenye Tuzo za Jomo Kenyatta Prize for Literature 2024.
Vitabu hivyo vinajumuisha ‘Dafina’ kilichoandikwa na Mutahi Mirisho, ‘Duara’ cha Dkt Timothy Arege na ‘Kifunganjia’ cha Daniel Okello. Vitabu hivyo vinashindania tuzo hizo katika kitengo cha Kiswahili (Watu Wazima).
Vitabu vinavyoshindana katika kitengo cha vijana ni ‘Mshale wa Matumaini’ (John Habwe), ‘Tumbo la Wageni’ (Wafula wa Wafula) na ‘Mkaidi’ (Gichimu Njeri).
Katika kitengo cha vitabu vinavyolenga watoto, kitabu cha ‘Swila Arejea na Hadithi Nyingine’ cha M.K. Tarus kitatuzwa bila mshindani.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Chama cha Wachapishaji wa Vitabu nchini (KPA) Kiarie Kamau, miswada ya vitabu iliyowasilishwa katika kitengo cha watoto, haikukidhi viwango vilivyowekwa.
Katika kitengo cha vitabu vya Kiingereza (Watu Wazima), vitabu vinavyomenyana ni ‘The Airlift Orphan’ (Marjory Kimani), ‘Mirror of the Blood’ (Patrick Ngugi) na ‘The Gambler’ (Ngumi Kibera).
Vitabu ‘The Maasai Mara Whisper’ (Gerald Kithinji), ‘A Jacket for Ahmet’ (Tony Mochama) na ‘The Case of the Prowling Panther’ (Gerald Kithinji) vinashindana katika kitengo cha vijana Kiingereza.
Mwaka huu hakuna kitabu kilichoorodheshwa kushindana katika kitengo cha watoto upande wa Kiingereza, na Tuzo ya Wahome Mutahi.
Tuzo ya Mutahi ilianzishwa kuyaenzi maisha ya mwandishi mahiri wa makala ya ucheshi marehemu Wahome Mutahi aliyeaga dunia mnamo 2003.
“Kati ya miswada iliyowasilishwa kwa ajili ya tuzo za Wahome Mutahi, hakuna hata kitabu kimoja kilichofikia vigezo vilivyowekwa,” akasema Bw Kamau.
Washindi watatangazwa na kutuzwa Septemba 29 -ambayo pia ni siku ya kufunga Maonyesho ya mwaka huu ya Vitabu yatakayong’oa nanga Septemba 25, Jumatano, katika jumba la Sarit Centre jijini Nairobi.
Kulingana na Bw Kamau, maonyesho hayo yamevutia washiriki kutoka nchi mbalimbali za kigeni kama vile China, Japan, Uingereza, Misri, Uturuki na Uajemi (Iran) kati ya mataifa mengineyo.
Zaidi ya washiriki 119 wataonyesha vitabu vyao katika hafla hiyo. Mwaka jana, zaidi ya watu 30,000 walizuru jumba la Sarit Centre kuhudhuria na kununua vitabu.
“Mwaka huu, tunatarajia zaidi ya Wakenya 35,000. Tutazindua vitabu kadhaa wakati wa maonyesho hayo. Wazazi, walimu, wanafunzi na maktaba zitakuwa na fursa mwafaka ya kununua vitabu,” akasema.