Habari za Kitaifa

Wabunge wanawake walaani kisa cha mwanamke kushambuliwa na ‘mijibaba’ mazishini  

Na MARY WANGARI March 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WABUNGE wanawake wamekemea vikali itikadi za jadi kitamaduni zinazoendeleza dhuluma dhidi ya wanawake kufuatia kisa ambapo mwanamke alishambuliwa kikatili katika hafla ya mazishi ya mumewe waliyetengana, Kaunti ya Nyamira.

Bi Mellen Mogaka alipokezwa kichapo cha mbwa na genge la wanaume waliomlazimisha kushiriki matambiko ya mazishi kwenye kijiji cha Nyamisimba, jinsi ilivyoonyweshwa kwenye video iliyosambazwa mitandaoni.

Wakihutubia vyombo vya habari Jumanne, Machi 25, 2025 katika majengo ya bunge, viongozi wanawake wakiwemo wabunge, maseneta na wawakililishi wanawake kupitia Muungano wa Wabunge Wanawake (KEWOPA) na Muungano wa Maseneta Wanawake (KEWOSA) walikashifu tukio hilo wakilitaja kama aina ya dhuluma za kijinsia (GBV) zinazoendelezwa na mila potovu zilizopitwa na wakati.

Aidha, wanasiasa hao wanaojumuisha Maseneta walioteuliwa Veronica Maina, Catherine Mumma, Karen Nyamu, Hamida Kibwana na wawakilishi wanawake Doris Donya na Betty Maina, walihoji ni vipi mama huyo alidhulumiwa hadharani mbele ya watoto wake huku umma ukitazama bila kumsaidia.

“Inasikitisha kundi la wanaume wahuni, kwa aina ya GBV ya kuchukiza mno, ya upumbavu uliokithiri na kukosa ustaarabu, walimshambulia wakisingizia kutekeleza mila za kitamaduni zilizopitwa na wakati,” walisema kupitia taarifa ya pamoja.

“Yote haya yalifanyika mchana peupe mbele ya wote waliohudhuria mazishi hayo na tunachukulia ikiwemo kanisa lililoongoza ibada, viongozi wa jamii na maafisa wa utawala.”

Seneta Mumma alielezea wasiwasi kuwa Wakenya hawazingatii tena jukumu la pamoja la kuwalinda wasio na nguvu za kujitetea katika jamii akisema, “Hatufai kutazama huku walemavu, wazee, wanawake na watoto, wakidhulumiwa siku nenda siku rudi, tunahitaji kuchukua hatua.”

“Viongozi na wazee wa jamii walikuwepo. Kisa hicho kilitendeka mbele ya maafisa wa serikali. Inasema mengi kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii yetu. Wanawake na watoto hawafai kudhulumiwa tukitazama. Mtu angewazuia wanaume hao kufanya walichofanya,” alisema Bi Mumma.

“Inahuzunisha kuwa watoto wa mwanamke huyu walipitia masaibu hayo. Hata ikiwa ni wa jamii ya Kisii, sijui wanawaza nini kuhusu jamii yao baada ya kushuhudia aliyopitia mama yao.”

Mwakilishi Mwanamke Migori, Fatuma Zainab alikosoa kanisa kwa kutazama mhasiriwa, watoto wake na mama yake mzazi wakidhulumiwa pasipo kuchukua hatua akisema tukio hilo limewasawiri wanawake wa Kenya kama wasio na thamani na ambao hakuna sheria inayowalinda.

“Ni dhambi kubwa sana kanisa likisimama pale likihubiri jinsi Yesu alivyofunza halafu wanamwacha mwanamke akipigwa,” alihoji Bi Zainab.

“Desturi gani hiyo inasaidia mwanamke lakini inahangaisha mwanamke. Desturi gani hiyo inayooegemea upande mmoja. Kama ni desturi kweli inafaa kumchunga mume na kumchunga mke.

“Tunaikashifu sana na tunauliza, dini yenu inafunza nini? Tunamsifu Yesu Kristo, lakini tunatazama mwanamke akishambuliwa. Tunakemea na kuuliza dini yenu inafunza nini?” Alitaka kujua Zainab.

Wabunge hao sasa wanaitaka Wizara ya Usalama wa Ndani inayoongozwa na Waziri Kipchumba Murkomen “kutangaza msimamo wake kuhusu suala hilo,” wahusika wakamatwe na mhasiriwa alipwe fidia.

Aidha, wametoa wito kwa wanawake wote kutoa habari kuhusu mila potovu zinazoendeleza GBV.