Wabunge washangaa IEBC kudaiwa deni la Sh4.9 bilioni na mawakili
WABUNGE wametaka maelezo kuhusu ni kwa nini Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inadaiwa jumla ya Sh4.9 bilioni na baadhi ya kampuni za mawakili walioiwakilisha katika kesi kadhaa za uchaguzi.
Pesa hizo pia zinajumuisha pesa ambazo IEBC ilitarajiwa kulipa baada ya kupoteza kesi mbalimbali dhidi yake mahakamani.
Hata hivyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Marjan Hussein Marjan, aliwaambia wabunge wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC) kwamba viwango vya ada zinazolipwa mawakili “ni vile vilivyokubaliwa.”
Wabunge waliambiwa kuwa Sh163 milioni kati ya kiasi chote cha fedha zinazodaiwa IEBC, ni pesa ambazo tume hiyo ilipaswa kulipa kutokana na maamuzi yaliyotolewa dhidi yake mahakamani.
Wanachama wa PAC Nabii Nabwera (mbunge wa Lugari) na mwenzake wa Mathioya Edwin Mugo walitaja kiasi hicho cha pesa (Sh4.9 bilioni) kama cha juu zaidi.
Walipendekeza kuwa kamati ya kuthibitisha madeni ambayo hayajalipwa inapasawa kuchambua madeni kabla ya IEBC kuyalipa.
“Kama ningekuwa Waziri wa Fedha na niambiwe nitoe kiasi hiki cha pesa kuwalipa mawakili, ningejivuta kufanya hivyo,” Bw Nabwera akasema.
“Je, tunajipata kuhitajika kulipa fedha nyingi kama ada za mawakili kwa sababu ya utepetevu au kukosa mawakili wa serikali? Mbona IEBC ilipe kiasi kikubwa kama hiki?” Bw Nabwera akauliza.
Naye Dkt Mugo akasema: “Tunahitaji ripoti ya kamati ya kuthibitisha madeni kabla ya fedha kama hizo kutolewa kwa kampuni za mawakili waliokodiwa na IEBC.”
Hata hivyo, Bw Marjan alitaja kiasi hicho cha fedha kama halali akisema ukodishaji wa mawakili kutoka nje uliidhinishwa na Afisi ya Mwanasheria Mkuu.
“Mawakili wetu hawangeweza kushughulikia idadi kubwa ya kesi za kupinga matokeo ya chaguzi mbalimbali zilizowasilishwa dhidi ya IEBC mahakamani,” Afisa huyo Mkuu Mtendaji akaiambia PAC Jumatatu, Agosti 26, 2024.
“IEBC ilitafuta ushauri kutoka kwa Mwanasheria Mkuu na akasema kuwa IEBC haiwezi kutumia mawakili walioko katika afisi yake. Alisema IEBC hutunga kanuni zake mahsusi kuhusu ukodishaji mawakili kutoka nje,” Bw Marjan akaambia kamati hiyo chini ya uongozi wa Mbunge wa Butere Tindi Mwale.
Bw Marjan alifichua kuwa tume hiyo ina mawakili wanne wanaoongozwa na Bw Chrispinus Owiye, mkurugenzi wa masuala ya kisheria.
Baada ya uchaguzi mkuu wa 2017, jumla ya kesi 301 za kupinga matokeo ya chaguzi za viti mbalimbali ziliwasilishwa mahakamani.
Kesi hizo zilijumuisha ile ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais na ambapo matokeo hayo yalibatilishwa.
Katika uchaguzi mkuu wa 2022, IEBC ilikumbwa na kesi 124 za kupinga matokeo ya chaguzi, ikiwemo ile ya kupinga matokeo ya urais na iliyofeli.
Baadhi ya kampuni za mawakili zinazoidai IEBC mamilioni ya fedha ni pamoja na Cootow and Associates (Sh20.52 milioni), Mukele Moni and Advocates (Sh17.2 million) kuhusu kesi tano za chaguzi zilizowasilishwa Nairobi, Garane and Somane Advocates (Sh55.6 million) na kampuni ya Kimani Muhoro and Advocates inayodai jumla ya Sh12.8 million.