Wabunge wataka sera ya kuhamisha walimu nje ya kaunti zao ifutiliwe mbali
WABUNGE wanataka sera ya kuwahamisha walimu iondolewe wakisema imesababisha kukosa usawa katika ajira na uhamisho wa walimu katika shule zote nchini.
Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Utekelezaji na uangalizi wa Katiba, (CIOC) inasema sera hiyo ambayo imetumiwa na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) tangu 2018, inaegemea upande mmoja na imesababisha ajira ya walimu kutoka maeneo mbalimbali nchini kukosa usawa.
Sera ya uhamisho ilihitaji TSC kuhamisha walimu kufunza katika maeneo yaliyo nje ya makazi yao asilia ili kuondoa hali ya maslahi kukinzana katika usimamizi wa shule za umma.
Hata hivyo, Kamati inayoongozwa na Mbunge wa Runyenjes, Erick Muchangi, ilisema katika kikao na TSC kwamba, sera hiyo haina msingi kisheria.
Bw Muchangi alisema maafikiano hayana nguvu kisheria na hayawezi kutumiwa na TSC kama kigezo cha kuajiri walimu.
“Hii ni kamati ya bunge kuhusu uangalizi wa Katiba. Ni sheria ipi mnatumia kwa sera hii?” Bw Muchangi aliuliza Afisa Mkuu Mtendaji, TSC, Nancy Macharia.
“Tunahitaji kutafuta sehemu kwenye sheria na hoja iliyopitishwa kama maafikiano ya Bunge,” alisema Bw Muchangi.
Bi Macharia, hata hivyo, alitetea TTSC akisema imepokea barua kutoka kwa Bunge kuhusu muafaka uliopitishwa kuhusu sera ya uhamisho.
“Muafaka ulipitishwa na bunge hili na nyinyi ni wabunge mnaounda sheria, mkitaka kuibadilisha, basi tupo tayari kuelekezwa na tutatekeleza mtakachosema,” alisema Bi Macharia.
Alisema kwa sasa, Tume imefungwa na muafaka wa Bunge akifahamisha wabunge kuwa, suala hilo limejitokeza mara kadhaa mbele ya Kamati za Elimu na Utekelezaji, ambazo zimejitolea kubadilisha sera ya utekelezaji.
“Kamati ya utekelezaji imekuwa ikifuatilia utekelezaji wa sera hiyo. Kumbuka nusra nifurushwe kwa sababu ya sera hii. Sasa nifanye nini?” aliuliza.