Wafanyabiashara Mlima Kenya walia kulazimishwa kufunga kazi kumshangilia Ruto
BAADA ya kile kilichotajwa kama kupokelewa vizuri kwa Rais William Ruto katika eneo la Mlima Kenya, baadhi ya wananchi wameachwa na hasira.
Wafanyabiashara katika kaunti za Laikipia na Kirinyaga wanahesabu hasara kubwa baada ya bidhaa zao kuharibika walipoamriwa kufunga biashara zao ili waende kumshangilia kiongozi wa nchi.
Katika soko la wazi la Nanyuki, wafanyabiashara wa nguo za mitumba pia waliathirika kwani vibanda vyao viko kando ya soko la mazao, kwenye barabara iliyotumiwa na msafara wa rais kuelekea mradi wa nyumba za bei nafuu.
Wakati wa ziara yake mnamo Aprili 1, 2025 shughuli za rais zilijikita katika eneo moja la takriban kilomita moja ambapo alizindua ujenzi wa darasa katika Shule ya Msingi ya Nanyuki DEB, kukagua ujenzi wa soko la kisasa, na kutembelea mradi wa nyumba za bei nafuu ambao uko asilimia 97 kukamilika.
Hata hivyo, ratiba hiyo iliwashangaza wengi, ikisababisha usumbufu mkubwa kwa wafanyabiashara waliolazimika kufunga biashara zao kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi.
“Hatukuwa na habari kwamba tungeondolewa kwenye vibanda vyetu ili kumlaki rais. Maafisa wa kaunti wakiwa na polisi waliwasili sokoni saa tatu asubuhi na kutuamuru tufunge biashara,” akumbuka Bi Elizabeth Nyawira.
Bi Nyawira anasema zaidi ya wafanyabiashara 1,000 walilazimika kukaa bila kazi kwa saa saba wakisubiri hadi jioni waliporuhusiwa kurudi baada ya Rais Ruto kuondoka.
“Baadhi yetu tunauza bidhaa zinazoharibika kwa haraka na tulipata hasara kubwa kwani tulikuwa tayari tumenunua mizigo yetu ya kila siku bila kufahamu kwamba hatungeruhusiwa kuendelea na biashara. Kulikuwa na fununu kuwa tungefidiwa na ofisi ya Mbunge wa eneo hili na Mwakilishi wa Kike, lakini baada ya siku mbili hakuna aliyetuambia iwapo tutalipwa,” anaongeza Bi Nyawira.
Kwa bahati mbaya, Rais Ruto alitarajiwa kutembelea soko hilo linaloendelea kuboreshwa kwa gharama ya Sh350 milioni, lakini wafanyabiashara wanasema ziara hiyo haijabadilisha chochote kwani hakuna tarehe maalum iliyotolewa kuhusu kukamilika kwa ujenzi huo.
“Rais alikaa ndani ya soko kwa chini ya dakika tano ambapo alituahidi kuwa lingekuwa tayari ndani ya miezi miwili. Alipotoka nje na kuzungumza akiwa juu ya gari lake, alijipinga mwenyewe akisema vibanda vipya vitakuwa tayari baada ya miezi mitatu,” alisema mfanyabiashara wa mazao Bw Leonard Karanja.
Mfanyabiashara mwingine, Bw Peter Wangai, alishangaa kwa nini viongozi wa eneo hilo walimshauri rais kukagua au kuzindua miradi midogo ambayo haifai hadhi yake na ambayo husababisha usumbufu kwa wafanyabiashara wadogo.
Wakati huohuo, wazee wa vijiji zaidi ya 100 waliokusanywa kutoka maeneo matatu ya Kaunti ya Laikipia Mashariki wakiahidiwa kulipwa Sh 2, 000 kila mmoja bado hawajalipwa baada ya siku tatu.
Katika Kaunti ya Kirinyaga, wafanyabiashara mjini Kagio walihesabu hasara baada ya ziara ya Rais Ruto eneo hilo.
Wafanyabiashara walisema kuwa maafisa wa serikali na polisi waliwalazimisha kufunga baa na biashara zingine ili kumkaribisha Rais aliyekuwa amewasili kuzindua mradi wa soko la kisasa wa Sh600 milioni.
“Maafisa wa utawala na polisi walipita kutoka biashara moja hadi nyingine wakituamuru tufunge,” alisema mmoja wa wafanyabiashara.
Walilalamika kwamba siku yao iliharibika kwani hawakuuza chochote kutoka asubuhi hadi jioni Rais alipoondoka.
“Tuliamriwa kufunga biashara asubuhi na kusubiri Rais ambaye aliwasili saa 11 jioni na kutuhutubia hadi saa 12 jioni. Wakati wote huo hatukufanya biashara yoyote. Tunarejea enzi za giza za utawala wa KANU ambapo Rais Moi aliwalazimisha watu kufunga shule na biashara ili kumkaribisha kwa nyimbo za sifa,” alisema mfanyabiashara mwingine.
Wafanyabiashara walilalamika kuwa kulikuwa na vitisho vingi wakati wa ziara ya Rais, wakisema hawakuridhika kabisa.
“Hii si haki. Tunawezaje kulazimishwa kufunga biashara zetu ili kumkaribisha Rais? Kwa nini tunalazimishwa kumuunga mkono? Hili litamletea madhara Rais Ruto,” alisema mfanyabiashara mmoja mjini Kagio.