Wahubiri wa makanisa ya Kiinjilisti watamaushwa na Kenya Kwanza
MAKANISA kadhaa ya kiinjilisti yaliyomuunga mkono Rais William Ruto wakati wa uchaguzi uliopita sasa yanakosoa waziwazi serikali yake, na kuashiria mabadiliko makubwa katika msimamo wao.
Mabadiliko hayo yamezua mijadala ndani na nje ya makanisa hayo yanapotathmini upya ukuruba wao na serikali ambayo hapo awali waliunga mkono.
Wakati wa uchaguzi wa urais wa 2022, viongozi wa makanisa hayo waliunga Dkt Ruto na serikali ya Kenya Kenya wakiamini ahadi zake za kufufua uchumi na kulinda haki za jamii.
Mahubiri pia yaliambatana na wito kwa waumini kumpigia kura Dkt Ruto, ambaye waliamini angetimiza ahadi zake.
Lakini miaka miwili tu katika utawala wake, mengi ya makanisa haya sasa yanaonyesha kufadhaika.
Masuala muhimu kama vile kupanda kwa gharama za maisha, migawanyiko ya kisiasa, kashfa za ufisadi na kukosekana kwa maendeleo katika kushughulikia dhuluma za kijamii kumesababisha viongozi wa makanisa kutoa maoni yao.
Katika video iliyosambaa mtandaoni, Mchungaji Teresia Wairimu wa Kanisa la Faith Evangelistic Ministry (FEM) ambako Rais Ruto huabudu mara kwa mara alikosoa utawala wa Kenya Kwanza.
“Tumechoka na kelele. Usijifanye kama uko vitani; jizatiti kutumikia taifa na watu waliokupigia kura,” alisema.
Mchungaji Tony Kiamah wa Kanisa la River of God alitoa maoni sawa na hayo akirejelea maandiko kusisitiza kutamauka kwake.
“Biblia inasema tutawatambua kwa matunda yao, na kwa hakika, hakuna tunda la Mungu hapa. Baba zetu wa kanisa lazima wakubali kwamba tulifanya makosa,” alisema.
Mtume William Kimani wa Kanisa la Kingdom Seekers aliangazia jinsi serikali ya sasa ambayo awali iliungwa mkono na umma kwa kuahidi kuwa na Mungu, sasa imepotea njia.
Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA