Habari za Kitaifa

Wakenya wametuchangamkia, vuguvugu la viongozi vijana lajipiga kifua

Na JUSTUS OCHIENG’ August 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wa Muungano mpya wa Kenya Moja unaohusisha na wanasiasa chipukizi wamesema kuwa wamepokelewa vyema kwenye ramani ya kisiasa nchini na kueleza matumaini ya kutamba dhidi ya wanasiasa wakongwe.

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Mbunge wa Saboti Caleb Amisi, Gathoni wa Muchomba (Githunguri) na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino wamesema muungano huo umepokelewa vizuri na wanapanga misururu ya mikutano kujivumisha zaidi.

“Nimeshangazwa na jinsi ambavyo Wakenya wamekuwa wakitupokea na kutushaajisha si nchini tu bali hata wanaoishi nchi za nje. Nawahakikishia kuwa tumesikia kile ambacho wamekuwa wakisema na tutafanya juu chini kuhakikisha tunatimiza matarajio yao,” akasema Bw Sifuna.

Bi Wa Muchomba naye alisema Kenya Moja ni muungano ambao umejikita katika kutatua changamoto za Wakenya na haugemei katika mrengo wowote wa kikabila.

“Sisi ni wabunge chipukizi kutoka vyama mbalimbali vya kisiasa na wenye fikira huru. Tumegundua kuwa nchi hii imekuwa ikifungwa kwenye uongozi wa viongozi wale wale wa vyama ambao hawajatupeleka mahala popote huku shida za Wakenya zikiendelea kuongezeka,” akasema Bi Wa Muchomba.

“Hatuwezi kuwaruhusu viongozi wakongwe wazamishe nchi, hawana maslahi ya Wakenya na kama viongozi chipukizi lazima tujitokeze na kuhakikisha nchi ipo kwenye mkondo mzuri wa uongozi,” akaongeza.

Bi Wa Muchomba ambaye pia amewahi kuhudumu kama mbunge mwakilishi wa kike wa Kiambu, alisema wao kwa sasa hawamakinikii siasa za 2027 ila watakuwa wakiitia serikali shinikizo itimize ahadi ilizotoa kwa Wakenya.

“Tunataka kuhakikisha vijana wanapata ajira, watoto wanapata elimu na kubadilisha ramani ya siasa zetu ambayo kila mara huchukua mkondo wa kikabila,” akasema Bi Wa Muchomba.

Mbunge huyo hata hivyo alisema kuwa bado wanatathmini hali na iwapo Wakenya wanataka waunde chama cha kisiasa na wawanie viti vyote mnamo 2027 basi wapo tayari.

“Wakenya wasirejeshe viongozi wakongwe tena 2027, Raila amekuwa waziri mkuu, Kalonzo makamu wa rais. Wataleta nini kipya ambacho hawajakifanya miaka hii yote wamekuwa serikalini,” akasema.

Bw Amisi naye alisema kuwa Kenya Moja ni karata ya kisiasa ambayo wamekumbatia bila kujali iwapo wataponzwa kisiasa.

“Tumechukua hatua hii kwa sababu watu wanaumia kimyakimya. Hata viongozi wengi serikalini wanaitetea hadharani lakini wakiwa kibinafsi, hawafanyi hivyo na wanatuambia utawala huu hauridhishi,” akasema Bw Amisi.

Kiongozi huyo alisema viongozi ambao wapo katika serikali ya sasa hawawezi kuongoza mageuzi na kurejesha taifa kwenye mkondo mzuri.

“Wakenya ndani na nje ambao wana ujuzi wa teknolojia, wamesoma, wana ujuzi wanataka kuongoza mageuzi nchini na lazima tufaulu. Iwapo hatutafanya hivyo, tawala zinazokuja zitakuwa kali sana kwetu na kutudhulumu,” akasema.

Kenya Moja sasa inapanga misururu ya mikutano Bumula, Saboti na Teso ambako itakuwa ikiendeleza michango kwa makundi mbalimbali ya akina mama.