Habari za Kitaifa

Wakulima North Rift wakwama na mahindi serikali ikipunguza bei

Na BARNABAS BII October 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAKULIMA wa mahindi katika eneo la North Rift wamekwama na mahindi ya mamilioni ya pesa kutokana na kushuka kwa bei ya zao hilo.

Wakulima waliokata tamaa ambao wanahodhi maelfu ya magunia ya mahindi kufuatia mavuno mengi kutokana na usambazaji wa mbolea ya ruzuku na hali nzuri ya hali ya hewa hawawezi kupeleka mazao hayo kwa Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) baada ya serikali kukosa kutenga fedha kwa ununuzi wa zao hilo.

Wakulima hao wanataka serikali itengee NCPB fedha chini ya bajeti ya ziada ili iweze kununua zao lao kwa bei ya juu ya Sh4,000 kwa gunia la kilo 90 ili kuwawezesha kupata faida.

“Ikitokea kwamba serikali haitatenga pesa za kununua mahindi chini ya bajeti ya ziada, mabroka watatumia kukata tamaa kwa wakulima kununua zao lao kwa bei ya chini na kuhifadhi mazao ili kusababisha upungufu sokoni,” alisema Kipkorir Menjo, Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima Kenya (KFA)

NCPB ilipunguza mahindi iliyonunua kwa magunia milioni 1 msimu uliopita ikitoa Sh4,000 kwa kila gunia jambo ambalo liliwafungia nje wakulima wengi wadogo kunufaika na mpango huo.

“Wakulima wanaweza kulazimika kurejea kuuza zao lao mitaani iwapo serikali haitaweka sera za wazi ikiwa ni pamoja na kutoa bei za kuvutia kusaidia kilimo ambacho kinajenga uchumi kwa kutenga fedha zaidi kununua zao hilo,” alisema Jackson Too, mkulima kutoka Moiben kaunti ya Uasin Gishu.

Kulingana na Waziri wa Kilimo Dkt Andrew Karanja, nchi inatazamia ongezeko la magunia 20 milioni ya kilo 90 ya mahindi msimu huu kutokana na utoaji wa mbolea ya ruzuku ya serikali, upatikanaji wa mbegu zilizoidhinishwa na hali nzuri ya hewa.