Wakulima walalamikia marufuku ya kuchuuza chai
WAKULIMA wadogo wa majani chai wameelezea wasiwasi wao kuhusu marufuku ya serikali dhidi ya uuzaji wa zao lao kwa wachuuzi.
Wanasema hatua hii imeathiri vibaya mapato yao, kwani wamekuwa wakitegemea njia hii kupata fedha za haraka kwa mahitaji ya kila siku.
Serikali imeanza msako dhidi ya wachuuzi hao kwa lengo la kuboresha ubora wa chai inayouzwa nje ya nchi.
Kwa mujibu wa barua ya Bodi ya Chai ya Kenya (TBK), marufuku imewekwa kwa uuzaji wa majani chai nje ya vituo rasmi vya KTDA.
TBK inasema kuwa wachuuzi wanachangia kupungua kwa ubora wa chai kwa sababu wanalenga wingi wa mavuno badala ya ubora unaohitajika.
Hata hivyo, wakulima wanasema kuwa marufuku hii inawanyima fursa ya kuuza chai kwa njia mbadala na kuwafanya kutegemea viwanda vya KTDA ambavyo hulipa mara moja tu kwa mwezi.
“Serikali ingetafuta njia ya kutusaidia kupata masoko bora badala ya kutufungia njia zetu za kipato,” alisema Bi Amina Juma, mkulima kutoka Kericho.
Philip Ngeno, aliyekuwa mkurugenzi wa KTDA, alitilia shaka uwezo wa TBK kutekeleza marufuku hiyo kwa ufanisi.
“TBK ina uwezo gani wa kutofautisha kati ya chai halali na ile inayouzwa moja kwa moja kwa wafanyabiashara?” alihoji.
KTDA ililipa wakulima Sh89.29 bilioni mwaka wa kifedha uliomalizika Juni 2024, ongezeko la Sh21.5 bilioni kutoka mwaka uliopita.
Hata hivyo, wakulima wanasema kuwa marufuku hii inawaweka katika hali ngumu ya kifedha. Wanaitaka serikali kushirikiana nao kutafuta suluhisho badala ya kuweka vikwazo ambavyo vinaathiri moja kwa moja ustawi wao wa kiuchumi.
Bw John Mwangi, anasema kuwa tangu marufuku hiyo ilipotangazwa, hali imekuwa ngumu zaidi.
“Tulikuwa tunategemea kuuza majani chai kwa wafanyabiashara, lakini sasa hatuna pa kuuza. Majani yanaharibikia mashambani, na hatuna njia nyingine ya kupata pesa za kulipa karo za watoto wetu au kukidhi mahitaji ya kila siku,” anasema kwa huzuni.
Viongozi wa wakulima pia wameelezea wasiwasi wao kuhusu athari za marufuku hiyo kwa uchumi wa jamii za mashambani. Wanasema kuwa hatua hiyo imeathiri sio tu wakulima, bali pia wafanyakazi wa mashamba, madereva wa kusafirisha majani chai, na hata biashara ndogo zinazotegemea sekta hiyo.
Baadhi wanasema kuwa badala ya marufuku, serikali ilipaswa kuanzisha mfumo wa kusaidia wakulima kupata masoko bora na bei nzuri kwa zao lao.
“Ikiwa kweli serikali inataka kulinda wakulima, inapaswa kuhakikisha kuwa viwanda vinanunua chai kwa bei nzuri na kuwasaidia kupata masoko ya moja kwa moja,” asema Bi Amina.