Habari za Kitaifa

Walimu, wanafunzi North Rift wasifia mchango wa ‘Taifa Leo’ katika kukuza Lugha ya Kiswahili

Na TITUS OMINDE July 8th, 2024 2 min read

MAADHIMISHO ya Siku ya Kiswahili duniani katika kaunti za North Rift yalitumiwa kusifia mchango wa ‘Taifa Leo’ katika ukuzaji wa lugha ya Kiswahili.

Walimu kwa wanafunzi walipongeza gazeti la ‘Taifa Leo’ na kampuni ya Nation Media Group kwa jumla kwa kujitolea kulea na kuboresha lugha ya Kiswahili.

“Tunaposherekea Siku ya Kiswahili Duniani (SIKIDU) tunapongeza gazeti la ‘Taifa Leo’ kwa kuwa gazeti la kipekee la Kiswahili ambalo linajali maslahi ya wanafunzi kwa walimu. Kupitia kwa gazeti hili matokeo ya somo la Kiswahili yameboreka shuleni mwetu,” alisema mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Paul Boit mjini Eldoret, Shem Busolo.

Akihutubu wakati wa maadhimisho ya SIKIDU shueleni humo, Bw Busolo alisema taaluma ya Kiswahili yapaswa kuboreshwa zaidi ili kuvutia wanafunzi zaidi.

Bw Busolo alisema tangu shule yake iaanze kutumia magazeti ya ‘Taifa Leo’ shuleni humo wanafunzi wengi wamekipenda Kiswahili huku akisema matokeo ya somo hilo yamezidi kuimarika kila uchao shuleni humo.

Kiongozi wa chama cha wanafunzi shuleni humo alikosoa pendekezo la wizara ya elimu la kutaka somo la Kiswahili liwe somo la hiari katika mtihani wa Kitaifa.

“Wanaopendekeza somo la Kiswahili kuwa la hairi wanatukosea, somo hili limekuwa chombo muhimu sana kwetu kama wanafunzi hivyo basi kulifanya somo la hiari ni kuua Kiswahili,” alisema mmoja wanafunzi wa shule ya upili ya Paul Boit Boys.

Naye mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Matunda SA, Mary Luvanda alisifia mchango wa wataalam wa lugha hiyo ambapo kwa sasa wanafunzi wengi shuleni mwake wanakienzi Kiswahili.

“Kiswahili kimekuwa lugha ya kujivunia hivyo basi nashukuru wataalam wa lugha hii kupanga siku ya leo kuwa sikukuu ya Kiswahili, kuna haja ya jamii kukumbatia lugha hii,” alisema Bi Luvanda.

Bi Luvanda pia alipongeza mradi wa magazeti masomomoni kupitia kwa gazeti la ‘Taifa Leo’, almaarufu NIE.

“Kiswahili kimesaidia wanafunzi wengi kuanza kuandika vitabu, hivyo basi somo hili limeibuka kuwa bora zaidi shuleni mwetu. Magazeti ya Nation Media hasa gazeti la ‘Taifa Leo’ limechangia kuboreka kwa matoeo ya lugha ya Kiswahili shuleni mwetu,” alisema Bi Luvanda.

Msimamizi wa idara ya Kiswahili shuleni humo Gabriel Mbeka alikosoa paendekezo la kutaka somo ya Kiswahili kuwa la hairi.

“Somo la Kiswahili lapaswa kuwa la lazima kuanzia shule ya chekechea hadi shule za upili; fununu za kufanya somo la Kiswahili kuwa la hiari haipaswi kusikika,” alisema Bw Mbeka

Bw Mbeka alihimiza kubuniwa kwa baraza la Kitaifa la Kiswahili ili liwe nguzo muhimu ya kukuza lugha ya Kiswahili.