Waombolezaji watimua Kuria kutoka mazishi ya Wanjigi
WAZIRI wa Utumishi wa Umma, Bw Moses Kuria Ijumaa alilazimika kukatiza hotuba yake katika mazishi ya aliyekuwa waziri Maina Wanjigi kaunti ya Nyeri baada ya waombolezaji kumzoma na kuimba nyimbo za kupinga serikali.
Waziri huyo alikuwa amezungumza kwa dakika mbili alipokatizwa vikali na kelele za waombolezaji walioimba nyimbo za kutaka serikali kuondoka mamlakani.
“Ruto must go,” waliimba kwa nguvu na kumfanya Kuria kuondoka jukwaani.
“Asante sana, ahsante sana,” Kuria alisema na kwenda kuketi akisindikizwa na kelele.
Waziri huyo alikatizwa alipokuwa akiwaambia waombolezaji kwamba nafasi ya Wanjigi katika historia ya Kenya haiwezi kufutika.
“Nimefika hapa kwa sababu historia ya taifa haiwezi kufutika. Katika historia ya nchi hii, jina la Maina Wanjigi haliwezi kusahaulika,” alisema kabla tu kelele kuanza.
Waziri huyo alilazimika kuondoka baada ya waombolezaji kuendelea kumzoma hata baada ya kukatiza hotuba yake.
Hata hivyo, maafisa wa usalama waliingilia kati haraka ili kuhakikisha usalama wa Kuria, na kumsindikiza mbali na eneo la tukio.
Hii ilisababisha mazishi kusitishwa kwa muda kabla ya kuanza tena.