Habari za Kitaifa

Watahiniwa wanne wa KCSE wazuiliwa kuhusu mauti ya mwenzao Shiners School Nakuru

Na MERCY KOSKEI November 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WANAFUNZI wanne katika Shule ya Upili ya Shinners, Kaunti ya Nakuru wanaendelea kuzuiliwa na polisi baada ya mwanafunzi mmoja mtahiniwa kudungwa kisu mnamo Jumamamosi usiku na akafa akikimbizwa hospitalini.

Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu John Mwangi alishikia vurugu na walipokimbia kuona kilichokuwa kikiendelea, walimpata mwanafunzi mmoja alikuwa amedungwa kisu tumboni.

Walimkimbiza hadi Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Nakuru lakini akaaga dunia njiani. Mwanafunzi mwengine ambaye pia alikuwa amedungwa kwenye paja la kushoto naye alitibiwa na kuruhusiwa kurejea shuleni.

Usimamizi wa shule ulipiga ripoti kuhusu kisa hicho kwenye kituo cha polisi cha Kiongorira na polisi wakafika shuleni kuanza uchunguzi.

“Inasikitisha kuwa tumempoteza mwanafunzi mwerevu na mwenye bidii. Uchunguzi unaendelea kuhusu kisa hiki,” akasema Bw Mwangi.

Mwalimu huyo mkuu alisema kuwa wakati wa tukio hilo, wanafunzi walikuwa wakijiandaa kuenda darasini kudurusu nyakati za jioni ili kujiandaa kwa mtihani wa Jumatatu ndipo vurugu hizo zikaanza.

Kiini cha mzozo huo kilikuwa ni vijana wanne ambao walikuwa wametimuliwa shuleni kwa wiki mbili, kisha wakarejea na kutaka kujua aliyekuwa amefungua masanduku yao.

Wanne hao walikuwa wameruhusiwa warejee shuleni ili wafanye mtihani wao wa KCSE. Mmoja ambaye anashukiwa alimdunga mtahiniwa mwenzake kisu hadi akafa ametoweka na inashukiwa aliwasili nyumbani kwao Nairobi.

“Tunasubiri mwelekeo kutoka Wizara ya Elimu ili tujua mahali ambapo watafanyia mtihani wao. Hatuwezi kuwaruhusu wakae hapa shuleni kwa sababu watahiniwa wenzao wana hasira na hilo linaweza kuleta janga jingine,” akaongeza Bw Mwangi.

Kwa mujibu wa Naibu Kamishina wa Kaunti Ndogo ya Gilgil Willy Cheboi mtahiniwa aliyetoroka hana maadili na ni mtovu wa nidhamu. Alisema uchunguzi unaendelea kuhusu kisa hicho na maafisa kutoka Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) wanahusika.

“Kumekuwa na tatizo na nidhamu ya wanafunzi katika shule hii ya Shiners. Walianza mtihani vyema kabla ya kisa hiki cha mauti na wale ambao wanazuiliwa na polisi watasaidia katika uchunguzi.

“Tunavyozungumza utulivu umerejea shuleni na tunatarajia mtihani utaendelea kama kawaida,” akaema Bw Cheboi.