Habari za Kitaifa

Watu kumi wafariki kwenye ajali ya lori na matatu mbili, 20 wajeruhiwa

Na RUSHDIE OUDIA November 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WATU 10 walifariki na wengine 20 kujeruhiwa katika ajali ya barabarani karibu na kituo cha kibiashara cha Iguhu – Yala Bridge kwenye Barabara ya Kakamega Kisumu.

Ajali hiyo iliyotokea mwendo wa saa kumi na mbili na nusu Jumatano jioni ilihusisha magari matatu – lori la kusafirisha mafuta ya petroli na matatu mbili za kubeba abiria 14.

Lori la kusafirisha mafuta lilikuwa likiendeshwa kutoka Kisumu kuelekea Kakamega na dereva asiyejulikana.

Alipofika eneo la ajali, dereva alipoteza udhibiti wa gari hilo na likageukia upande wa kulia wa barabara kuelekea Kakamega.

Liligonga magari mawili aina ya Toyota moja ya chama cha matatu cha Mitrans Sacco lililokuwa likiendeshwa na dereva ambaye hakutambuliwa mara moja lililobeba abiria ambao idadi haikujulikana mara moja na nyingine ya Transiline Sacco iliyokuwa na abiria 14.

Matatu zilikuwa zikiendeshwa kutoka Kakamega kuelekea Kisumu.

Kulingana na walioshuhudia, dereva wa lori hilo alipoteza udhibiti na gari lililogonga matatu hizo mbili.

Walijaribu kuwaokoa majeruhi lakini kwa bahati mbaya baadhi walikuwa tayari wamefariki na wengine walikuwa wamenaswa kwenye mabaki ya magari hayo.

“Kutokana na ajali hiyo, watu 10 walikufa papo hapo na 20 wakajeruhiwa. Timu yangu ilitembelea eneo la tukio, kupiga picha na kuanza uchunguzi,” ilisema ripoti ya tukio la polisi kutoka Afisi Trafiki eneo la Magharibi.

Miili ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali kuu ya Kaunti ya Kakamega kusubiri kutambuliwa huku majeruhi wakikimbizwa katika Hospitali ya karibu kwa matibabu.

Magari hayo yalivutwa hadi kituo cha Polisi cha Kakamega.

Dereva wa lori hilo alitoroka baada ya ajali hiyo.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA