Habari za Kitaifa

Watu wawili wa familia moja wafariki baada ya kuruka nje ya matatu iliyopata hitilafu za breki

Na GEORGE MUNENE January 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

JAMAA wawili wa familia moja waliaga dunia huku watu wengine wanne wakipata majeraha mabaya Alhamisi Januari 2, 2025 wakati waliporuka nje ya matatu ilipopata matatizo ya breki kwenye mteremko.

Waliopoteza maisha yao ni mama na bintiye ambao walikuwa wanaenda hospitali ya Kerugoya kwa matibabu.

Kulingana na walioshuhudia kisa hicho, abiria waliingiwa na hofu wakati matatu hiyo ilipokumbwa na hitilafu za breki na dereva akashindwa kuidhibiti katika eneo la Kibingo, kwenye barabara ya Kerugoya – Kutus.

Gari hilo lilikuwa linaelekea Embu likitokea Karatina na ajali hiyo ilisababisha msongamano mkubwa katika eneo hilo.

Huku matatu hiyo ikishuka mteremko ikiyumbayumba, baadhi ya abiria walianza kuruka nje wakipiga mayowe na kuanguka kwenye lami kichwa kwanza, jambo lililosababisha mmoja wao kufariki papo hapo.

Hata hivyo, gari hilo lilisimama wakati lilipoanguka kwenye shamba la kahawa, kilomita tano kutoka eneo lilipoanza kupata matatizo ya breki.

Walioponea walikimbizwa katika hospitali ya Kerugoya.

“Abiria waliokuwa wamejawa na hofu waliruka nje ya gari ambalo lilikuwa kwenye mwendo wa kasi, na kwa bahati mbaya wawili walipoteza maisha yao,” akasema John Kiama, afisa wa kitengo cha kukabiliana na majanga katika Kaunti ya Kirinyaga.

Wakazi waliopigwa na butwaa walikuwa wamedhania kwamba gari hilo lilitekwa nyara kwa sababu abiria walikuwa wakipiga mayowe kwa nguvu.

“Tulikuwa tukifanya shughuli zetu karibu na eneo la ajali wakati tulipoona gari likishuka kwa kasi sana na tukadhani lilikuwa limetekwa nyara kwa sababu ya mayowe ya abiria. Baadaye tulibaini kwamba ni breki zilikatika na kusababisha hofu kubwa miongoni mwa abiria,” mkazi mmoja akasema.

Abiria tisa na dereva waliobaki ndani waliondoka salama bila majeraha.

Gari hilo lilipelekwa katika kituo cha polisi cha Kerugoya ambapo polisi wanasema dereva huyo anaweza kushtakiwa kwa kuendesha gari lisilo katika hali shwari ya kimitambo.