Habari za Kitaifa

Yafichuka Ikulu imejitwika jukumu la ‘kuajiri’ walimu wanasiasa wakitumika kusambaza barua za kazi 

Na WINNIE ATIENO na NIVAH KIRIMI April 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MADAI ya mbunge mwakilishi wa kike Kaunti ya Murang’a, Betty Njeri Maina, kuwa wabunge wanaoegemea serikali majuzi walipatiwa barua za kazi ya walimu kwa wakazi wa maeneobunge yao kinyume cha sheria, yamezua balaa kuhusu mchakato haramu wa ajira.

Vyama vya walimu vimelalamikia hatua hiyo vikisema inawanyima Wakenya wanaostahili fursa ya kuajiriwa huku taifa likikumbwa na kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira miongoni mwa walimu waliohitimu.

“Tuliitwa Ikulu na nitasema wazi. Tulipatiwa barua za (kuajiri) walimu. Nilienda na wabunge 11 kutoka Kiambu, na kila mmoja alipatiwa barua 20, zikiwa jumla ya barua 220,” alisema Bi Maina.

“Kutoka Murang’a, tulienda pamoja na mbunge wa Mathioya, Dkt Edwin Mugo. Ninajua hapa eneobunge la Maragua, kuna walimu ambao bado wanasubiri kazi. Mbunge wenu ni rafiki yangu. Nitamburura na kumrejesha kwa serikali ili mpate maendeleo,” Bi Maina alifichua siri kuhusu mtindo unaoendelea.

Alidai wabunge ambao hawakujitokeza Ikulu walifeli wakazi kutoka maeneobunge yao ambao hawatapata nafasi za kazi za kufunza.

Aliyekuwa Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu aliwahi kunaswa na kamera akimpa barua ya ajira mwalimu ambaye hakuwa ameajiriwa kwenye mkutano wa hadhara kaunti ya Kisii.

Mwaka jana, 2024, Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse, aliyejipatia umaarufu baada ya kuwasilisha hoja ya kumfurusha aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua, alijitapa kuhusu ushawishi wake katika ibada ya mazishi eneobunge lake Desemba 14 2024.

“Zungumzeni baina yenu na mtambue mwalimu aliyefuzu na aliye tayari kufunza katika shule ya sekondari ya Muatini. Mnipe jina lake kabla ya hafla hii kukamilika ili aajiriwe Jumatatu na kuanza kufunza papo hapo. Mlishangaa mbona nilijiunga na serikali. Mtu ambaye hayupo serikalini anaweza kuajiri mwalimu mazishini?” Alihoji.

Jumapili, Aprili 2, 2025, kaimu katibu mkuu wa chama cha walimu wa shule za sekondari (Kuppet), Moses Nthurima na naibu katibu mkuu wa Chama cha Walimu Nchini (Knut), Hesbon Otieno, walionya kwamba kuajiri walimu nje ya mchakato unaoruhusiwa kisheria kutaathiri sekta ya elimu.

Walitahadharisha serikali dhidi ya kuingiza siasa kwenye sekta ya elimu wakisema Ikulu haina mamlaka ya kuajiri walimu.

“Tafakari wakati wabunge wanawachagua marafiki na jamaa zao kuajiriwa. Ilhali waliokamilisha chuo cha mafunzo 2016 wangali wanasubiri kuajiriwa kwa haki. Utaajiriwa kwa sababu unamfahamu mwanasiasa? Ni taswira gani tunachora?” Alisaili Bw Nthurima.

Bw Otieno alisema mtindo huo utahujumu kanuni za ajira katika TSC na kusababisha ukosefu wa usawa katika usambazaji wa walimu kote nchini.

“Shughuli za TSC hazifai kuingizwa siasa. TSC ni taasisi ya kitaaluma. Ina majukumu yanayojumuisha kuajiri na kuteua wafanyakazi,” alisema.

Tungali hatujabaini jinsi barua za ajira zinavyoishia mikononi mwa wanasiasa.

Mkurugenzi wa mahusiano kisheria, leba na kiviwanda TSC, Cavin Anyuor, hakujibu simu na jumbe zetu kuhusu suala hilo.