Yafichuka Raila anakutana na mawaziri ‘wake’
WAZIRI Mkuu wa zamani Raila Odinga anaonekana kuendesha vikao vyake vya mawaziri wanaotoka chama chake cha ODM mbali na vile rasmi vya baraza la mawaziri wote vinavyoongozwa na Rais William Ruto.
Bw Odinga na Rais Ruto wametia saini mkataba wa ushirikiano ambapo waliorodhesha masuala 10 ya kushughulikia, japo walisisitiza kuwa hawajagawana mamlaka.
Huku Rais Ruto akiongoza vikao vya baraza la mawaziri, Bw Odinga amekuwa akikutana na wale wa kutoka chama chake kwa mashauriano.
Alhamisi, Machi 20, 2025 alikutana na mawaziri wanne wanachama wa ODM na viongozi wengine wa mrengo wake bungeni saa chache kabla ya Rais kubadilisha makatibu wa wizara.
“Nilikutana na wataalam wetu katika Muungano Jumuishi pamoja na viongozi wetu bungeni kushauriana kuhusu masuala ya kitaifa na yanayoibuka,” Bw Odinga alisema kupitia anwani zake za mitandao ya kijamii baada ya mkutano huo.
Katika mkutano huo, Raila alikutana na Waziri wa Nishati Opiyo Wandayi, Waziri wa Madini na Uchumi wa Majini Hassan Joho, Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya, Waziri wa Fedha John Mbadi, na Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Askul Moe ambao amekuwa akiwarejelea kama wataalamu aliochangia serikali inyooshe utawala.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA) Ndiritu Muriithi, Kiongozi wa Wachache bungeni Junet Mohamed, na Kiongozi wa Wachache katika Seneti Stewart Madzayo.
Bw Muriithi pia ni mshauri wa masuala ya kiuchumi wa Bw Odinga huku Junet na Madzayo wakiwa wanachama wa ODM.
Machi 7, 2025, Odinga alitia saini mkataba wa kushirikiana na chama cha UDA cha Dkt Ruto, hatua ambayo imevunia washirika wake nafasi katika serikali ya Kenya Kwanza.
Baada ya makubaliano hayo, uongozi wa kamati za bunge umeshuhudia mabadiliko makubwa, huku wabunge wa ODM wakichukua nyadhifa ambazo kwa kawaida huhifadhiwa kwa chama tawala, kama vile uenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Matumizi ya Fedha, ambayo sasa inaongozwa na Mbunge wa Alego-Usonga Samuel Atandi, aliyemrithi Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.
Katika mkutano wa Alhamisi, zaidi ya washirika 10 wa Bw Odinga waliteuliwa makatibu wa wizara tofauti katika hali inayothibitisha hadhi yake mpya serikalini.
Wachambuzi wa siasa wanasema kila hali inaonyesha Raila ni mshirika sawa katika serikali japo hashikilii wadhifa unaojulikana kisheria.
“Kwa sasa Kenya ina serikali ya nusu mkate ambayo inathibitishwa na uteuzi unaofanywa kama wa juzi wa makatibu ambapo ODM ilipewa nafasi nyingi. Kwa kuwa kwa sasa hakuna wadhifa anaotoshea Bw Raila, anashauriana na washirika wake ili wamweleze kinachoendelea ndani ya serikali,” akasema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.
“Bila shaka Raila hawezi kutegemea mawaziri wa mrengo wa Rais Ruto japo hivi karibuni unaweza kuona wakimtembelea kwa kuwa ushawishi wake katika serikali hii unaongezeka,” aongeza Dkt Gichuki.