Hali si shwari: Waiguru ayumbishwa na kimbunga cha siasa
Na WANDERI KAMAU
GAVANA wa Kirinyaga, Anne Waiguru wa Kirinyaga amejipata tena katika utando wa kisiasa, hali inayohatarisha kipindi alichobakisha kuhudumu kama gavana.
Kwa muda wa miezi saba pekee ambayo amehudumu kama gavana, Bi Waiguru amejipata katikati ya mawimbi makali ya kisiasa, wadadisi wakionya kwamba huenda yakayumbisha merikebu yake kisiasa.
Kisa cha Ijumaa, ambapo baadhi ya wakazi walimpigia kelele kwenye mkutano uliohutubiwa na Naibu Rais William Ruto wakimtaka kutowahutubia, kiliashiria upeo wa uhasama wa kisiasa ambao umekuwepo kati yake na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake, Bi Wangui Ngirichi.
Kufikia sasa, Bi Waiguru anakabiliwa na kesi inayopinga kuchaguliwa kwake iliyowasilishwa na Bi Martha Karua (Narc-Kenya), ambapo juhudi zake za kuiomba mahakama isisikizwe tena zimeambulia patupu.
Kisiki kingine kinachomwandama ni madai ya baadhi ya viongozi, kwamba amekuwa akiyatenga baadhi ya maeneo kimaendeleo.
Katika kisa hicho, majibizano makali yalizuka kati yake na Bi Wangui Ngirici, ambapo Bi Waiguru alimlaumu (Ngirici) kwa kuwalipa vijana ili kumpigia kelele.
“Ngirici na mumewe (Andrew) ndio waliohusika katika njama za kuwalipa vijana ili kusambaratisha mkutano wa Bw Ruto na ajenda zangu za maendeleo,” akasema Bi Waiguru.
Hata hivyo, Bi Ngirichi alimjibu vikali, akikanusha ufahamu wowote wa njama hizo.
“Anapaswa kutoa ushahidi wowote alio nao ikiwa nilihusika katika vitendo anavyodai. Sitakubali mtu aniharibie jina bila thibitisho,” akasema Bi Ngirichi.
Wawili hao wamekuwa katika vita vikali vya kisiasa, ambapo Bi Ngirici amekuwa akiendesha miradi yake ya maendeleo kupitia kundi la Ngirici Rescue Team, ambako amekuwa akimlaumu Bi Waiguru kwa kutotimiza ahadi alizotoa kwa wakazi.
Katika kesi ya Bi Karua, juhudi za Bi Waiguru kuisimamisha mahakama ziligonga mwamba, mahakama ikishikilia kwamba ni haki ya mlalamishi katika kesi hiyo kusikilizwa tena.
Kutatua matatizo
Kwa hayo mchanganuzi wa kisiasa Ndegwa Njiru anasema kwamba itabidi viongozi wa sasa katika kaunti hiyo kutatua matatizo hayo, ili kumrahisishia kazi gavana huyo.
“Ingawa changamoto hizi huenda zikaonekana kumkabili Bi Waiguru, uhalisia ni kwamba mwananchi ndiye atakayeumia. Hivyo, ni muhimu sasa kwa viongozi kushauriana,” asema Bw Njiru.
Masaibu hayo yanamtokea Bi Waiguru aliyechaguliwa kama gavana baada ya kulazimika kujiuzulu hapo awali kama Waziri wa Ugatuzi katika Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kutokana na sakata ya madai ya ufisadi katika Huduma ya Kitaifa kwa Vijana (NYS).
Katika sakata hiyo, inakisiwa kwamba karibu Sh791 milioni zilipotea katika hali tatanishi, ila Bi Waiguru amekuwa akishikilia kuwa hakuhusika kwa vyovyote vile.
Baadhi ya wachanganuzi pia wanasema kuwa ni wakati mzuri kwa serikali kuingilia kati ili kuzuia mgawanyiko zaidi katika kaunti hiyo muhimu.