HabariSiasa

Hamtatuweza, Ruto na Waiguru wafokea wakosoaji

August 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

NAIBU Rais William Ruto na Gavana wa Kirinyaga, Bi Anne Waiguru Alhamisi walikemea vikali wanaowahusisha na ufisadi wakisema ni watu ambao wamehisi kushindwa kisiasa.

Walitaja matokeo ya kura ya maoni yaliyotolewa na shirika la Ipsos kama “injili ya shetani” na “mbinu chafu zilizopitwa na wakati.”

Walisema jana walipokutana katika nyumba rasmi ya Naibu Rais mtaani Karen, Nairobi,

Mkutano wa wawili hao uliofanyika katika makazi rasmi ya Bw Ruto, mtaani Karen, Nairobi na kuhudhuriwa na madiwani wa wadi zote katika kaunti ya Kirinyaga, ulifanyika siku moja tu baada ya ripoti ya utafiti wa shirika la Ipsos kudai Wakenya wengi wanaamini viongozi hao wawili ndio fisadi zaidi nchini.

Ripoti hiyo iliyotolewa Jumatano ilionyesha kuwa, asilimia 33 ya Wakenya wanaamini Bw Ruto ndiye mwanasiasa fisadi zaidi nchini, akifuatwa kwa karibu na Bi Waiguru kwa asilimia 31.

Lakini jana, Bw Ruto alipuuzilia mbali ripoti hiyo akisema ni “injili ya shetani” inayoenezwa na watu wasioamini kuwa mtoto wa maskini anaweza kutia bidii maishani hadi akatajirika bila kujihusisha kwa ufisadi.

Kulingana naye, ripoti zinazoenezwa kila mara kumhusisha na ufisadi huchochewa na wapinzani wake wa kisiasa ambao wanafahamu amewashinda kwa rekodi ya maendeleo ya kitaifa.

“Tumewashinda kwa namna tunavyohudumia Wakenya, sasa wameamua kutoa ripoti feki za utafiti. Kusema kweli, hawatawahi kushinda rekodi zetu za maendeleo,” akasema Bw Ruto.

Wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo ya utafiti, mtafiti mkuu wa Ipsos, Bw Tom Wolf, alisema walifuata kanuni zote za utafiti wa kisayansi kwa hivyo matokeo hayo ni ya kuaminika kusheheni maoni ya Wakenya kwa jumla. Naibu Rais alitaka wapinzani wake waendeleze siasa za kimaendeleo akisema siasa duni hazina manufaa kwa wananchi.

“Hatutakubali waturudishe kwa ulingo wa kisiasa usio na manufaa kwa Wakenya,” akasema.

Kwa upande wake, Bi Waiguru ambaye kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na sakata ya ufisadi katika shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS) alipokuwa Waziri wa Ugatuzi, alisema uchunguzi ulifanywa dhidi yake na ikabainishwa kuwa hakuwa na hatia ilhali wapinzani wake bado humwandama kwa sakata hiyo. Alitishia kufichua watu waliohusika katika uporaji wa pesa za umma katika shirika hilo ikiwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) haitafanya hivyo.

“Sijawahi kuiba hata peni moja kutoka kwa umma. Hawa ni watu ambao wanataka kujipanga kisiasa kwa hivyo wameonelea watumie vita vinavyoendelezwa dhidi ya ufisadi kusukuma ajenda zao za kisiasa. uwekeni siasa kando,” akasema.

Tangu Rais Kenyatta alipoanza kukaza kamba kupambana na ufisadi, wandani wa Ruto wamekuwa wakilalamika kuwa juhudi hizo zinalenga kuhujumu nafasi ya kushinda urais mnamo 2022. Kwa upande wake, utawala wa Bi Waiguru umekuwa ukikumbwa na misukosuko Kirinyaga ambapo kumeibuka makundi ya wakosoaji wanaotishia umaarufu wake.

Wawili hao baadaye walielekea katika Ikulu ambapo Rais Uhuru Kenyatta aliongoza hafla ya kutuza wanawake waliotoa mchango mkubwa kwa taifa, na kuzindua kitabu kilichoandikwa na Mbunge wa zamani wa Karachunyo, Bi Phoebe Asiyo.