Hatimaye wanasayansi wagundua dawa inayoangamiza HIV
Na ANGELA OKETCH
MATUMAINI ya kupatikana kwa dawa ya Ukimwi yameongezeka baada ya matokeo ya utafiti kwa dawa inayofahamika kama Gammora, kuonyesha inaweza kuangamiza hadi asilimia 99 ya virusi vya HIV mwilini mwa binadamu kwa kipindi cha wiki nne.
Matokeo hayo yaliyotolewa wikendi, yalionyesha kuwa Gammora ilipunguza sana virusi vya HIV mwilini mwa binadamu kwa kuangamiza seli inayobeba maambukizi hayo mwilini, bila kudhuru seli za mwilini ambazo hazijashambuliwa na virusi hivyo.
Hii ni tofauti na dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARVs) zinazotumika kwa sasa ambazo huzuia tu ueneaji wa virusi hivyo mwilini.
Utafiti huo ulifanywa na watafiti kutoka kampuni ya Zion Medical nchini Israeli, kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Hebrew mjini Jerusalem.
“Dawa hii hufanya seli iitwayo apoptosis, iliyoshambuliwa na HIV ijiue. Ina uwezo wa kutibu wagonjwa walioambukizwa HIV kwa kuangamiza seli zote zinazobeba HIV. Matokeo ya majaribio ya kwanza yalitushangaza kwani hayakutarajiwa, na yameleta matumaini makubwa kuhusu kupatikana kwa tiba ya ugonjwa huo,” akasema Dkt Esmira Naftali, mkuu wa ustawishaji katika Zion Medical.
Aliongeza kuwa wagonjwa tisa katika Hospitali ya Ronald Bata Memorial iliyo nchini Uganda walichaguliwa kupokea viwango tofauti vya dawa hiyo kama tiba kwa kati ya wiki nne na tano.
Kwenye majaribio ya pili yaliyofanywa wiki mbili baadaye, wagonjwa walipewa dawa hiyo pamoja na nyingine ya kupunguza makali ya Ukimwi kwa kipindi sawa na hicho cha muda.
Matokeo yake yalionyesha kuwa mchanganyiko wa dawa ulipelekea kiwango cha virusi mwilini kupungua kwa hadi asilimia 99 kwa muda wa wiki nne za kupokea tiba bila kuonyesha madhara yoyote ya kiafya.
Kwenye utafiti huo uliofanywa kwa wiki kumi, wagonjwa wote kwenye makundi mawili waliongeza kiwango cha seli za CD4 ambazo huwa ni muhimu kwa kinga mwilini.
Prof Abraham Loyter wa Chuo Kikuu cha Hebrew alianzisha utafiti huo miaka kumi iliyopita.
Awamu nyingine inatarajiwa kuanza karibuni kwa kuongeza idadi ya wagonjwa watakaohusishwa kufika 50, na kipindi cha kupokea tiba kitaongezwa hadi miezi mitatu.
Kwa kawadia dawa mpya haziwezi kutumiwa hadi zifanyiwe utathmini na kuidhinishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).
Nchini Kenya, tafiti zinaonyesha kuna wananchi zaidi ya milioni 1.5 ambao wameambukizwa Ukimwi ingawa maambukizi mapya yamekuwa yakipungua.