Kimataifa

Hoteli inayowapa wateja 'bunduki' kukabiliana na ndege wasumbufu

June 5th, 2018 1 min read

VALENTINE OBARA Na MASHIRIKA

PERTH, AUSTRALIA

HUKU Serikali ya Kaunti ya Mombasa ikipanga kutumia Sh30 milioni kuangamiza kunguru wasumbufu, hoteli iliyo Australia imevumbua njia ya kuzuia ndege wengine wasumbufu kuhangaisha wageni wake.

Kulingana na mashirika ya habari, hoteli iliyo katika eneo la Perth, Australia, huwapa wageni wake bunduki bandia za kurushia ndege wa baharini maji ili kuwafukuza wanapokula ufuoni.

Mmiliki wa hoteli ya 3Sheets, Bw Toby Evans, alinukuliwa kusema kuwa ndege hao wanaofahamika kama ‘seagulls’ huhangaisha sana wageni na ilibidi hatua zichukuliwe dhidi yao.

Ilisemekana kila meza huwekewa bunduki hizo za maji na kufikia sasa wateja wameridhishwa na uwezo wao kuwafurusha ndege hao kwa njia ambayo pia huwaburudisha.

Bila shaka, wawekezaji katika sekta ya utalii Mombasa wanaweza kuiga mbinu hii au wavumbue mbinu zingine bora zaidi za kukabiliana na kunguru wakorofi.