Habari

ICC yazua baridi mpya kwa UhuRuto

July 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

WASIWASI kuhusu kufufuliwa kwa kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), umeibuka upya.

Hii ni baada ya kufichuka kuwa aliyekuwa wakili wa waathiriwa wa ghasia hizo, Fergal Gaynor ana nafasi bora zaidi kuchukua mahali pa Bi Fatou Bensouda, ambaye anatarajiwa kukamilisha hatamu yake Juni 2021.

Tayari Kenya imepinga orodha ya walioteuliwa kuwania wadhifa huo ikisema mtu mmoja anapendelewa.

Katika barua iliyofichuliwa Jumatano, Balozi wa Kenya nchini Uholanzi ambako ni makao makuu ya ICC, Bw Lawrence Lenayapa, aliambia mahakama hiyo kwamba Kenya inapinga majina ya walioteuliwa kumrithi Bi Bensouda.

Ijapokuwa Bw Lenayapa hakutaja mteuliwa ambaye Kenya inaamini anapendelewa kuwa mkuu mpya wa mashtaka, wataalamu wa sheria za kimataifa wanasema ni wazi Kenya ina wasiwasi endapo Bw Gaynor atamrithi Bi Bensouda.

Kwa msingi wa kuwakilisha waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini, Bw Gaynor ana ufahamu mkubwa kuhusu kesi zote za Kenya.

Ijapokuwa kesi za Rais Kenyatta na Dkt Ruto zilisitishwa kwa madai kwamba hapakuwa na ushahidi wa kutosha , majaji wa ICC walitoa fursa kwa Afisi ya Kiongozi wa Mashtaka (OTP) kuzifufua tena endapo wapelelezi wataridhishwa kwamba wamepata ushahidi mpya ulio na uzito.

Wasiwasi wa Kenya ni kuwa iwapo Bw Gaynor atapewa kazi hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa kufufua kesi dhidi ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto, ikizingatiwa alikuwa wakili wa waathiriwa wa ghasia za 2007/08.

Bw Mark Kersten, ambaye ni mtaalamu wa sheria za kimataifa, alisema wasiwasi wa Kenya hauhusu utaalamu wa watu walioteuliwa kujaza nafasi ya Bi Bensouda mbali kesi kufufuliwa.

“Kesi zile za awali hazifai kutumiwa kama kigezo cha kuamua ufaafu wa wakuu wa mashtaka wanaoteuliwa. Naamini malalamishi ya Kenya yametokana na kuwa Morris na Gaynor walihusika katika kesi za Kenya. Wale walioshtakiwa bado wako mamlakani na wana wasiwasi kuhusu uwezekano wa ICC kufufua kesi za Kenya,” akasema.

Ripoti za kila mwaka kutoka kwa afisi ya Bi Bensouda huonyesha kwamba, licha ya kesi kusitishwa, wapelelezi wa ICC bado huzuru Kenya mara kwa mara kuendeleza ukusanyaji wa ushahidi mpya kuhusu kesi za ghasia zilizoua watu zaidi ya 1,300 na kuacha maelfu wengine bila makao hadi leo hii.

Mnamo Januari 2020 Dkt Ruto alisema anafahamu kuhusu mipango ya kufufua kesi hizo, tena akadai ni kati ya njama za kuzima maazimio yake ya kumrithi Rais Kenyatta ifikapo mwaka wa 2022.

Hata hivyo, ICC ilipuuza madai yake ikasema uamuzi wa korti mnamo 2016 ulikuwa wazi kwamba kesi zinaweza kufufuliwa ushahidi ukipatikana, na shughuli za mahakama hazifai kuingiziwa siasa.

Kando na Bw Gaynor, wengine walioteuliwa ni Bi Susan Okalany kutoka Uganda, Bw Richard Roy ambaye ni raia wa Canada na Bw Morris Anyah wa Nigeria, ambaye pia aliwakilisha waathiriwa wa ghasia za Kenya katika ICC kwa muda mfupi.

Mtaalamu wa sheria za kimataifa, Bw Astrid Coracini, alieleza kuwa ni desturi katika mashirika ya kimataifa kwamba nyadhifa kubwa hushikiliwa kwa mzunguko kutoka kwa ukanda mmoja hadi mwingine, hali inayomweka Bw Gaynor katika nafasi bora zaidi kupata kazi hiyo.

Hivyo basi, kutokana na kuwa Bi Bensouda ni Mwafrika aliye raia wa Gambia, itakuwa vigumu kushawishi mataifa kumchagua mwafrika kwa mara nyingine kumrithi.

Kwa upande mwingine, Naibu Mkuu wa Mashtaka aliye mamlakani kwa sasa ni raia wa Canada, Bw James Stewart, kwa hivyo haitawezekana kumchagua Bw Roy kujaza nafasi ya mkuu wa mashtaka.