Habari

IEBC yasema iko tayari kuandaa chaguzi ndogo ikiwa Uhuru atavunja bunge

October 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imesema iko tayari kuendesha chaguzi ndogo za ubunge na useneta endapo Rais Uhuru Kenyatta atavunja bunge kulingana na ushauri wa Jaji Mkuu David Maraga.

Prof Abdi Guliye ambaye ni mmoja wa makamishna wa tume hiyo Ijumaa aliambia kamati ya Seneti kuhusu Uwiano wa Kitaifa na Usawa kwamba tume hiyo itaendesha kibarua hicho endapo itafadhiliwa.

“Tume iko tayari. Tuko na zaidi ya wafanyakazi 900 katika kaunti zote 47 na maeneobunge 290. Kwa hivyo, tunaweza kuendesha chaguzi ndogo. Usaidizi ambao tutahitaji ni wa kifedha,” Prof Guliye akasema alipofika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Seneta Maalum Naomi Shiyonga.

Tofauti na karatasi za sita za kura ambazo huhitajika katika uchaguzi mkuu, uchaguzi mdogo utakaofanywa utahitaji karatasi za kiti cha ubunge, Mwakilishi wa Wanawake na Seneta.

Hata hivyo, Prof Guliye alidinda kutaja gharama ya chaguzi hizo ndogo akisema hiyo itakadiriwa tu baada ya uamuzi wa kuvunjwa kwa bunge kufanywa.

“Gharama hiyo itakadiriwa baada ya viti hivyo kutangazwa wazi. Na bila shaka serikali ina mianya ya kisheria itakayoweza kutumia kuwezesha kupatikana kwa fedha za kuendesha chaguzi ndogo. Wakati huu tunajiandaa kwa uchaguzi mdogo katika eneobunge la Msambweni na wadi zingine nne,” akasema.

Alikuwa akiwajibu maseneta Samson Cherargei (Nandi) na Christopher Lang’at (Bomet) ambao walitaka kujua ni kwa nini IEBC iko tayari kwa chaguzi ndogo ilhali pesa hizo hazijatengwa katika bajeti ya mwaka huu.

“Mbona unasema mko tayari kwa chaguzi ndogo wakati huu ilhali hakuna fedha zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu kufadhili shughuli hiyo?” akauliza Bw Cherargei.

“IEBC inahitaji pesa ngapi ili iweze kuendesha chaguzi ndogo kujaza nafasi 290 za ubunge, 47 za useneta na 47 za Wabunge Wawakilishi wa Wanawake?” akauliza Bw Lang’at.

Septemba 2020, Maraga alimshauri Rais Kenyatta kuvunja bunge kwa kufeli kupitisha sheria ya kufanikisha uwepo wa usawa wa kijinsia katika asasi za uongozi ambazo wanachama wazo huchaguliwa na zile ambazo wanachama wazo huteuliwa.