Habari

Jenerali Badi atoa kauli yake kuhusu Sonko

July 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

BENSON MATHEKA na COLLINS OMULO

MKURUGENZI wa Idara ya Huduma za Nairobi (NMS), Meja Jenerali Mohamed Badi, hatimaye amevunja kimya chake kuhusu malalamishi ya Gavana Mike Sonko dhidi ya idara hiyo.

Katika kikao cha wanahabari afisini mwake mnamo Jumanne, Bw Badi alikosoa hatua ya Bw Sonko kupeleka malalamishi yake mahakamani kuhusu usimamizi wa kaunti.

Gavana huyo alikuwa amelalamika kwamba NMS, ambayo iko chini ya afisi ya Rais Uhuru Kenyatta, ilitwaa majukumu zaidi ya yale manne ambayo alikubali kusalimisha.

“Sitaki kujadili hili suala kwa mapana kwa sababu kuna kesi mahakamani. Lakini ninachoweza kusema ni kwamba makubaliano yanatoa nafasi ya kuunda jopo la kutatua mizozo. Nadhani hilo ndilo lingefanywa badala ya kukimbia mahakamani,” akaeleza.

Alikanusha madai ya Sonko kwamba amemzuia kutumia nyumba rasmi ya gavana, akisema shirika lake linataka kuikarabati kwanza.

Bw Badi alimkumbusha Bw Sonko kwamba masuala yote ya ardhi na nyumba yako chini ya NMS na anafaa kukoma kudai shirika hilo linamzuia kuingia nyumba hiyo.

“Nyumba ambayo gavana alienda haijakuwa ikitumiwa kwa zaidi ya miaka miwili. Ikiwa gavana anataka kuitumia, asubiri tuikarabati tunavyofanyia nyumba nyingine za kaunti,” Bw Badi alisema.

Wiki jana, Bw Sonko alimlaumu Bw Badi kwa kukataa atumie nyumba hiyo iliyoko mtaani Lavington.

Vilevile, Bw Badi alikanusha madai ya Gavana Sonko kwamba NMS imegeuza Nairobi kuwa himaya ya kijeshi akisema wafanyakazi wote wa shirika hilo wametumwa na Tume ya Utumishi wa Umma (PSC).

“Miongoni mwa wafanyakazi zaidi ya 7,000 wa NMS, kuna wanajeshi sita tu kwa hivyo ni makosa kusema wanajeshi wanasimamia jiji,” alisema.

Kwingineko, kizaazaa kilizuka katika bunge la kaunti ya Nairobi wakati polisi walipowarushia hewa ya kutoa machozi madiwani waliokuwa wakijaribu kumkabidhi Spika Beatrice Elachi ilani ya kumuondoa ofisini.

Madiwani hao walilazimika kutimua mbio kujinusuru polisi walipowazuia kuingia ofisi ya Bi Elachi aliyesemekana alikuwa amejifungia ndani.

Wawakilishi Wadi hao walikuwa wakitaka kumkabidhi spika pia agizo la kusimamisha uteuzi wa karani mpya wa bunge la kaunti, Edwin Gichana, pale polisi walipowazuia kuingia ofisi ya Bi Elachi.

Waligombana na maafisa hao waliokuwa wamejihami kwa silaha kabla ya hali kubadilika wakarushiwa hewa ya kutoa machozi.

Wanahabari walijipata katika kizaazaa hicho huku diwani wa Mlango Kubwa Patricia Mutheu akijeruhiwa kila mtu alipokuwa akitoroka kujinusuru.

Diwani wa Waithaka Antony Kiragu alisema fujo zilizuka spika alipokataa kukabidhiwa mswada na agizo hilo kwa sababu anafahamu akipokea atakuwa amesimamishwa kazi hadi mswada huo ujadiliwe na uamuzi kuafikiwa.

“Tangu Elachi aliporudi, kumekuwa na fujo na amekuwa akisimamia bunge kama mali yake binafsi,” alisema.

Bi Elachi alikuwa amedai kwamba shinikizo la kuondolewa kwake linatoka kwa Bw Sonko, kwa vile gavana huyo hataki kuwe na mabadiliko ya karani wa bunge na pia anataka kuhangaisha viongozi wanaounga mkono NMS.