HabariHabari za KauntiHabari za Kitaifa

Pepo la mauti laangamizi waumini wengine 25

Na PIUS MAUNDU NA WINNIE ATIENO October 26th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

SAFARI ya kurudi Mombasa baada ya mazishi ya askofu mwenzao iligeuka kuwa janga kwa wachungaji na familia zao baada ya basi walilokuwa wakisafiria kugongana ana kwa ana na lori katika eneo la Kanga, karibu na Mtito Andei, barabara kuu ya Mombasa-Nairobi.

Watu 25 waliaga dunia katika ajali hiyo ya saa mbili kasorobo asubuhi, huku manusura wakisimulia matukio ya mwisho, juhudi za kuokoa wenzao na maumivu ya kutofahamu hatima ya jamaa zao waliokuwa safarini.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa dereva wa basi hilo lenye uwezo wa kubeba abiria 52 alikuwa ameliendesha kwa zaidi ya saa 16 bila msaada wa dereva mwingine, jambo lililozua wasiwasi kuhusu uchovu na usalama barabarani.

“Dereva aliendesha gari kutoka Lugari, Kaunti ya Kakamega, hadi hapa. Hakuwa na mtu mwengine wa kumsaidia. Lazima alikuwa amechoka,” akasema Mchungaji Cosmas Nyangweso, mmoja wa manusura. Alisema aliona basi likianza kuyumba barabarani kabla ya kugongana na lori lililokuwa likitoka upande wa pili.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, basi hilo lilikuwa likijaribu kuyapita magari mengine lilipopoteza mwelekeo. Kamishna wa Kaunti ya Makueni, Abdullahi Khalif, alisema basi liliteleza na kuingia upande wa pili wa barabara kabla ya kugongana na lori, na kusababisha sehemu kubwa ya paa lake kung’oka.

Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) ilisema ripoti za awali zinaashiria kuwa magari hayo yaligongana ana kwa ana na huenda kuyapita magari mengine isivyofaa kulichangia ajali hiyo.

Basi hilo lilikuwa likirejea Mombasa baada ya abiria kuhudhuria mazishi ya Askofu Isaiah Kiganane katika kijiji cha Marakusi, Kakamega mnamo Jumamosi.

Askofu Zachariah Mwagandi, mkuu wa Kanisa la Glorious River International, alisema wachungaji walijadiliana iwapo warudi Mombasa siku hiyo hiyo baada ya mazishi. Hatimaye waliamua kuondoka saa kumi jioni na kusafiri usiku kucha.

“Tulikuwa na furaha tulipoondoka Mtito Andei baada ya kupata kifungua kinywa mwendo wa saa moja asubuhi. Tulikubaliana kuenda moja kwa moja nyumbani kwa askofu marehemu, ambako safari yetu ilianzia Alhamisi,” akasema.

Hata hivyo, furaha hiyo ilikatizwa na ajali iliyotokea dakika 15 tu baada ya kuondoka Mtito Andei.

Mchungaji Spenza Mdave wa Kanisa la Voice of Faith, Malindi, alisema manusura walilazimika kushirikiana na dereva kuwatoa wenzao kwenye mabaki ya basi, huku baadhi ya madereva waliopita wakipuuza kilio chao cha kuomba msaada.

“Tulishirikiana na dereva kuwaokoa manusura. Wengi wa waliofariki walikuwa wameketi nyuma ya basi,” alisema akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mtito Andei.

Hata hivyo, Bw Mdave alikuwa na wasiwasi kuhusu watoto wake wanne waliokuwa safarini.

Alisema alianza safari akiwa na watoto wake watano, lakini mmoja alishuka Nairobi huku wengine wakisisitiza kuendelea hadi Malindi kumwona mama yao.

Violet Mwandonyi, jamaa wa askofu marehemu, pia hakuwa na taarifa kuhusu watoto wake wawili waliokuwa kwenye basi hilo.

Katika Kaunti ya Mombasa, habari za vifo ziliwaacha waumini na familia katika majonzi. Mchungaji Joseph Vura wa Kanisa la Campaign for Salvation and Healing alikuwa amempigia msaidizi wake saa 6:45 asubuhi akimwambia atachelewa kufika kwenye ibada.

“Wakati wa simu alikuwa na furaha sana na aliniambia kuhusu safari na wachungaji aliokuwa nao. Sikujua alikuwa akinitumia ujumbe wa mwisho,” akasema Mchungaji Andrew Mjomba.

Baadaye, Bw Mjomba alipata habari kwamba Vura alikuwa miongoni mwa waliofariki. Mchungaji Isaac Juma wa Kanisa la Grace Healing Centre pia aliaga dunia.

Mchungaji Isaac Wangila wa Kanisa la Glory Worship Centre alisema zaidi ya wachungaji 30 waliondoka Mombasa kuenda Kakamega kuhudhuria mazishi hayo. Alisema Mchungaji Stephen Ouma alikuwa amejeruhiwa kifuani na kichwani, huku wachungaji watatu kutoka Bangladesh wakiripotiwa kufariki.

Jukwaa la Wahubiri Mombasa limeiomba serikali kuwasafirisha kwa ndege manusura wanaohitaji matibabu maalumu, kuondoa au kulipia bili za hospitali na kusaidia familia kugharamia mazishi.

Ajali hiyo imezua tena wito wa kupanuliwa kwa barabara ya Mombasa-Nairobi, wiki tatu tu baada ya mahujaji 17 Wakatoliki kufariki katika ajali nyingine karibu na Salama.

Mkurugenzi mkuu wa NTSA, Nashon Kondiwa, alisema ajali za barabarani zimefikia kiwango cha dharura kitaifa, huku watu 5,000 wakipoteza maisha kila mwaka.

Alisema kutangaza ajali za barabarani kuwa janga la kitaifa kungewezesha serikali kuunganisha juhudi za usalama, kuongeza ufadhili na kuweka malengo yanayopimika ya kupunguza vifo.