Jubilee yamtangaza Mariga mgombea wake wa ubunge Kibra
Na CHARLES WASONGA
CHAMA cha Jubilee kimemteua mwanasoka McDonald Mariga Wanyama kuwa mgombea wake katika uchaguzi mdogo katika eneobunge la Kibra mnamo Novemba.
Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) ya chama hicho Andrew Musangi alisema Jumatatu kwamba uamuzi huo ulifikiwa baada ya kuwahoji watu 16 waliosaka tiketi hiyo.
“Baada ya kuwahoji kwa makini jumla ya watu 16 waliotuma maombi ya kutaka kuwa wawaniaji wa kiti cha ubunge cha Kibra kwa tiketi ya Jubilee, bodi yangu umemteua Bw McDonald Mariga Wanyama. Hii ni kwa sababu tumeridhika kuwa ana ufahamu wa hali ya eneobunge hilo, ameonyesha bidii, nguvu na kujituma; sifa ambazo Jubilee inahitaji kwa mpeperusha bendera yake,” Bw Musangi akasema kwenye kikao na wanahabari saa moja usiku katika makao makuu ya Jubilee, mtaani Pangani, Nairobi.
Sasa ni rasmi kwamba Bw Mariga atakupambana na mgombeaji wa ODM ambaye atajulika Jumamosi baada mchujo wa chama hicho.
Vilevile, atakabana koo na mgombeaji wa chama cha Amani National Congress (ANC) Eliud Owalo na wagombeaji huru kadhaa.
Kiti cha Kibra kilisalia wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge Bw Ken Okoth mnamo Julai 26, 2019 katika Nairobi Hospitali baada ya kuugua kansa ya utumbo.
Umri
Bw Mariga mwenye umri wa miaka 32 amewahi kuichezea timu ya taifa Harambee Stars na miamba wa soka nchini Italia Inter Milan.
Vilevile, amewahi kuchezea timu zingine duniani miongoni mwao ikiwa ni Real Sociedad, Parma, Helsingborge na Real Oviedo.
Wengine waliong’ang’ania tiketi ya Jubilee kwa kinyang’anyiro hiki ni pamoja na Morris Kinyanjui, Walter Trenk, Ibrahim Said, Doreen Wasike, Oscar Kambona, Bukachi Chapia, Jane Githaiga, Jack Owino, Omondi Rajab, Daniel Adem, Daniel Orogo, Ramadhan Hussein, Fank Amollo, Timothy Kaimenyi na Geoffrey Mwangi.