Habari

Kang'ata ashikilia msimamo wa Jubilee kumwondoa Kindiki hauyumbishwi

May 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

KIRANJA wa wengi katika Seneti Irungu Kang’ata amepuuzilia mbali madai ya baadhi ya maseneta na wabunge kwamba hoja ya kumwondoa mamlakani Naibu Spika Kithure Kindiki imechochewa kisiasa.

Kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge Alhamisi jioni, Bw Kang’ata amesema hoja imewasilishwa kwa sababu “Kindiki amedharau chama.”

Hii ni baada ya seneta huyo wa Tharaka Nithi kufeli kuhudhuria mkutano wa kundi la maseneta wa Jubilee ulioitishwa na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi.

“Chama kimekosa imani na Naibu Spika. Alichelea kusema ni kwa nini hakuhudhuria mkutano huo; na hilo ni kosa kubwa zaidi,” Bw Kang’ata ambaye ni Seneta wa Murang’a amewaambia wanahabari.

Hata hivyo, kiranja huyo amedinda kufichua yule atakayepewa wadhifa wa Profesa Kithure, akisema wakati huu lengo kuu la Jubilee ni kuhakikisha kuwa ameondolewa ofisini.

“Wakati huu tunaelekeza macho yetu katika mjadala wa hoja hiyo kesho (Ijumaa) na upigaji kura. Baadaye chama kitaamua yule ambaye atachukua nafasi yake,” Bw Kang’ata akasema.

Seneta wa Uasin Gishu na mwenzake wa Nairobi wamekuwa wakipigiwa upatu kama wale ambao huenda mmoja wao akapewa wadhifa huo.

Hata hivyo, duru zinasema kuwa wawili hao hawajachangamkia cheo hicho, hali ambayo imefanya Jubilee kuanzisha mazungumzo na chama cha ODM kuhusu uwezekano wa kiti hicho kupewa mmoja wa maseneta wake.

Wale ambao majina yao yametajwa kama wanaofikiriwa kupewa kiti hicho ni Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo na Seneta Maalum Judy Pareno.

Na huenda hatima ya Profesa Kindiki tayari imeamuliwa baada ya Bw Kangata kufichua kwamba jumla ya maseneta 49 wametia saini hoja hiyo; ishara kwamba wanaiunga mkono.

Maseneta 27 wanatoka mrengo wa Jubilee na 22 wanatoka mrengo wa ‘Nasa’ wenye vyama tanzu vya ODM, Wiper na ANC.

Kulingana na kipengee cha 106 (2) (c) cha Katiba, hoja ya kumfuta kazi Naibu Spika sharti iungwe mkono na angalau thuluthi mbili ya idadi jumla ya maseneta ambayo ni 67.

Hii ina maana kuwa ni maseneta 45 wanaohitajika kupitisha hoja hiyo iliyowasilishwa rasmi katika seneti mnamo Jumanne asubuhi.

Profesa Kindiki ni mwandani wa karibu wa Naibu Rais William Ruto na ambaye wakati mmoja alipigiwa debe kuwa mgombea mwenza wake katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Hoja hii dhidi ya Profesa Kindiki inajiri wiki mmoja baada ya mwenzake wa Elgeyo Marekwet Kipchumba Murkomen kutimuliwa kutoka wadhifa wa Kiongozi wa Wengi na nafasi hiyo kutunukiwa Seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio.

Bw Kang’ata alipewa wadhifa wa Kiranja wa Wengi katika mkutano huo uliofanyika Ikulu ya Nairobi, baada ya kubanduliwa kwa Seneta wa Nakuru Susan Kihika.

Mnamo Jumatano Seneta wa Meru Mithika Linturi aliwaongoza wabunge kadha kutoka kaunti za eneo la Mlima Kenya Mashariki waliolaani hoja dhidi ya Profesa Kindiki.

“Tunajua kuwa mwana wetu anadhulumiwa kwa sababu za kisiasa; eti kwa sababu anaunga mkono mrengo fulani. Hii sio haki ikizingatiwa kuwa eneo letu la Mlima Kenya Mashariki lilimuunga mkono Rais katika chaguzi za 2013 na 2017,” akasema Bw Linturi.

Wabunge 12 wa mrengo wa ‘Tangatanga’ pia walipinga hoja hiyo wakisema ni njama pana ya kuzima ndoto ya Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta ifikapo mwaka 2022.