Habari

Kaunti 47 zinatarajiwa kupata Sh457.28 bilioni katika mgao mpya

Na COLLINS OMULO October 31st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

KAUNTI 47 zinatarajiwa kupata Sh457.28 bilioni kama mgao wa mapato ya kitaifa katika mwaka wa kifedha wa 2027/2028, ikiwa pendekezo la Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) litapitishwa.

Kiasi hicho ni ongezeko la Sh29.28 bilioni ikilinganishwa na Sh428 bilioni ambazo kaunti zilitengewa katika mwaka huu wa kifedha utakaokamilika Juni 30, 2027.

CRA, inayoongozwa na Bi Mary Chebukati, inapendekeza Wizara ya Fedha itengee serikali za kaunti fedha hizo katika mwaka unaoanza Julai 2027 na kukamilika Juni 2028.

Akizungumza na wanahabari Alhamisi, Bi Chebukati alisema pendekezo hilo linatokana na makadirio ya mapato ya kitaifa ya Sh3.24 trilioni yatakayogawanywa kati ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti.

Kati ya fedha hizo, serikali ya kitaifa inapendekezwa kupata Sh2.78 trilioni, huku kaunti zikitengewa Sh457.28 bilioni. Zaidi ya hayo, Sh10.25 bilioni zinapendekezwa kutolewa kupitia Hazina ya Usawazishaji.

Bi Chebukati alisema ongezeko hilo litasaidia kulipia mishahara ya wahudumu wa afya wanaotekeleza mpango wa afya kwa wote (UHC), pamoja na nyongeza ya mishahara kwa maafisa wa serikali na wafanyakazi wa umma katika awamu ya nne ya mapendekezo ya Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC).

Fedha hizo pia zinalenga kutekeleza makubaliano ya mishahara na marupurupu ya wauguzi, na kuongeza kwa asilimia tatu uwezo wa kaunti kutoa huduma kwa wananchi.

“Pendekezo hili linalenga kusawazisha mahitaji ya kifedha ya ngazi zote mbili za serikali, kuhakikisha matumizi endelevu, kulipa madeni ya umma na kudumisha utoaji wa huduma kwa Wakenya,” alisema.

Alisema mgao unaopendekezwa kwa kaunti ni sawa na asilimia 22.3 ya mapato ya kitaifa yaliyokaguliwa na kuidhinishwa hivi majuzi. Kiwango hicho ni zaidi ya kiwango cha chini cha asilimia 15 kinachotakiwa na Katiba.

Hata hivyo, pendekezo hilo linatolewa wakati ambapo Baraza la Magavana (CoG) linalalamikia kuchelewa kwa serikali ya kitaifa kutoa Sh8.9 bilioni zilizotengwa kulipia mishahara ya wahudumu wa mpango wa UHC walioajiriwa na kaunti kwa masharti ya kudumu na pensheni.

Mwenyekiti wa CoG, Muthomi Njuki, alisema kaunti zimelazimika kutafuta fedha kutoka kwa vyanzo vingine ili kuwalipa wafanyakazi hao.

Gavana huyo wa Tharaka Nithi alisema kaunti zimekuwa zikilipa wahudumu hao kwa miezi minne bila kupokea fedha ambazo serikali ya kitaifa iliahidi kutoa.

Serikali ya kitaifa kupitia Wizara ya Afya na serikali za kaunti zilikubaliana kuwa wahudumu hao wataajiriwa na kaunti, huku fedha za kugharamia mishahara yao zikifuata kupitia mgao wa ziada kwa serikali za kaunti.

Hata hivyo, Bw Njuki alisema fedha hizo bado ziko katika wizara ya fedha kwa sababu taratibu zinazohitajika ili kuzitoa hazijakamilishwa katika Seneti.

“Fedha zilizopaswa kutengewa kaunti bado ziko wizara ya fedha kwa sababu taratibu zinazohitajika kuzitoa hazijashughulikiwa katika Seneti,” alisema.

Alitaka fedha hizo zitolewe mara moja, akionya kuwa kucheleweshwa zaidi kunaweza kudhoofisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Wakati huo huo, CRA imependekeza kuongeza kiwango cha matumizi ya kawaida ya mabunge ya kaunti hadi Sh50.36 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2027/2028, kutoka Sh39.19 bilioni za sasa.

Hilo ni ongezeko la Sh11.17 bilioni, ambalo linalenga kugharamia mishahara ya madiwani (MCAs), shughuli za kawaida, magari, mafunzo na ajira za ziada.

Kati ya fedha hizo, Sh3.54 bilioni zitatumika kulipa mishahara na marupurupu ya wafanyakazi, Sh1.74 bilioni kwa shughuli na ukarabati, Sh4.81 bilioni kwa magari, Sh474 milioni kwa mafunzo na Sh597 milioni kutekeleza mfumo mpya wa ajira.

Kwa upande wa serikali kuu za kaunti, CRA imependekeza matumizi ya kawaida ya Sh25.85 bilioni, ikiwa ni ongezeko la Sh602 milioni pekee.