Habari

Maelfu ya majengo hatarini kuporomoka nchini, uchunguzi wabaini

Na SAMWEL OWINO October 31st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MAELFU ya Wakenya wanaoishi au kufanya kazi katika majengo mbalimbali nchini wako hatarini baada ya ripoti mpya kufichua kuwa zaidi ya nusu ya majengo yaliyokaguliwa hayakidhi viwango vya ujenzi.

Ripoti ya ukaguzi wa ubora kutoka Idara ya Ujenzi wa Umma, iliyowasilishwa bungeni, inaonyesha kuwa asilimia 57 ya majengo yaliyokaguliwa yana kasoro za kimuundo zinazoweza kusababisha mengi kuporomoka.

Kati ya majengo 21,282 yaliyokaguliwa kati ya Julai 1, 2025 na Aprili 2, 2026, ni 9,264 pekee, sawa na asilimia 43.53, yaliyopatikana kuwa salama na kukidhi masharti ya ujenzi. Majengo 12,018 hayakufuata viwango vilivyowekwa kisheria.

Hali hiyo imezua wasiwasi kuhusu usalama wa wananchi, hasa ikizingatiwa kuwa nchi imeshuhudia majengo 100 yakiporomoka tangu 1996.

Mwaka huu pekee, majengo manane yameporomoka, idadi kubwa zaidi kurekodiwa katika mwaka mmoja kulingana na ripoti hiyo.

Nairobi, ambayo hivi karibuni ilishuhudia jengo likiporomoka eneo la Eastleigh, ilikuwa na kiwango cha asilimia 57. Kati ya maeneo 3,908 ya ujenzi yaliyokaguliwa, ni 2,261 yaliyokidhi masharti.

Uliokuwa mkoa wa magharibi uliongoza kwa usalama, ukiwa na kiwango cha asilimia 77. Kati ya majengo 1,520 yaliyokaguliwa 1,183 yamejengwa kwa kufuata viwango vinavyotakiwa.

Kaskazini Mashariki ilikuwa na hali mbaya zaidi, ikiwa na kiwango cha utiifu cha asilimia tano pekee. Kati ya majengo 220 yaliyokaguliwa, ni 11 tu yaliyoruhusiwa kuendelea na ujenzi huku miradi 209 ikisitishwa.

Eneo la juu la Mashariki ya nchi lilifuata kwa asilimia 14, huku eneo la Kati ya Bonde la Ufa likiwa na asilimia 18.38, Pwani asilimia 20.25 na Nyanza ya Kati asilimia 20.68.

Eneo la Mlima Kenya lilikuwa na kiwango cha asilimia 65. Kati ya maeneo 1,225 yaliyokaguliwa, miradi 807 ilikidhi masharti huku 418 ikisitishwa.

Ripoti inasema kuporomoka kwa majengo kunachangiwa zaidi na kasoro katika usanifu, vifaa duni na kazi isiyozingatia viwango.
Baadhi ya wajenzi wa majengo wanadaiwa kupunguza gharama kwa kutumia saruji isiyotosha, hasa katika maeneo yenye udongo dhaifu, ili kuongeza faida.

“Baadhi ya wasanidi, katika juhudi za kupunguza gharama za ujenzi kwenye maeneo yenye udongo dhaifu, huathiri kiwango na ubora wa saruji, na hivyo kuongeza hatari ya majengo kupata hitilafu za kimuundo na kuporomoka,” ripoti inasema.

Pia kuna watu wasiohitimu wanaojifanya wahandisi na wasanifu majengo, wanaouza michoro ya ujenzi kwa wawekezaji.

Ripoti inasema baadhi ya wakandarasi hutumia wafanyakazi wasio na ujuzi, kupuuza michoro iliyoidhinishwa na kukwepa taratibu muhimu kama kuchanganya saruji kwa vipimo sahihi, kubana na kuimwagilia maji kwa muda unaotakiwa ili ikauke vizuri.

Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi (NCA) ina jukumu la kukagua maeneo ya ujenzi na kuhakikisha yanafuata sheria. Wakaguzi huangalia iwapo mkandarasi amesajiliwa, ana cheti, vibali vimebandikwa kwenye bango la mradi na wataalamu wanaohusika wameidhinishwa.

Pia hukagua vifaa vya kujikinga kwa wafanyakazi, mabango ya usalama, uzio wa eneo la ujenzi na iwapo wasimamizi pamoja na wafanyakazi wana vyeti vinavyotambulika.

Mradi unapopatikana kukiuka masharti, NCA inaweza kusimamisha ujenzi na kuweka alama nyekundu ya X kuonyesha kuwa kazi hairuhusiwi kuendelea hadi kasoro zirekebishwe.

Mwenye jengo hupewa siku 14 kutekeleza masharti yanayotolewa. Akishindwa, anaweza kufunguliwa mashtaka mahakamani.

Mtu anayepatikana na hatia ya kukaidi agizo la mkaguzi anaweza kufungwa jela miaka mitatu, kutozwa faini ya Sh1 milioni au adhabu zote mbili.

Hata hivyo, ripoti inaonyesha kuwa kufikia Machi 31, 2026, ni kesi 15 pekee zilizokuwa zimefanikiwa katika kaunti mbalimbali.

Ripoti inalaumu uchunguzi na mashtaka machache kwa kuchochea hali ya kutowajibika miongoni mwa wawekezaji na wataalamu wasiofuata maadili. Inataka idara za usimamizi na uchunguzi kuimarishwa ili wanaokiuka sheria wawajibishwe.

Miradi yote inapaswa pia kufuata Kanuni za Ujenzi za 2024, zinazoweka viwango vya usanifu, ujenzi na utunzaji wa majengo. Kanuni hizo zinataka michoro na usimamizi wa ujenzi kufanywa na wataalamu waliosajiliwa katika taaluma husika.

Wanaokiuka masharti hayo wanaweza kutozwa faini ya Sh1 milioni, kufungwa jela au kupokonywa leseni zao za kitaaluma na za kuwa wanakandarasi.

Ripoti inasema Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) pia huchunguza kwa kina visa vya majengo kuporomoka ili kubaini iwapo kuna makosa ya jinai yaliyofanyika.