Habari

Kesi dhidi ya mbunge wa zamani yagonga mwamba

October 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Mbunge wa Tetu na mwenyekiti wa Kamati ya Usalama na Uhusiano wa Kimataifa Bungeni, James Ndung’u Gethenji alifikishwa mahakamani Jumatano, lakini kesi aliyokusudiwa kufunguliwa iligonga mwamba baada ya wafanyakazi wake wanne kukosa kufika kortini.

Wakili Ishmael Nyaribo anayemwakilisha mshtakiwa akiwa na Nelson Osiemo na Willis Otieno, alimsihi hakimu mwandamizi Bw Bernard Ochoi aahirishe kesi hiyo hadi Oktoba 28.

“Kesi hii dhidi ya Ndung’u inatokana na mzozo mkali kuhusu udhibiti wa mtaa wa kifahari wa Kihingo Village (Waridi Gardens) Limited (KHWGL) wenye thamani ya Sh20 bilioni,” alisema Bw Nyaribo.

Wakili huyo alimweleza hakimu kuwa Ndung’u anazozana na nduguye mkubwa Bw Fredrick Gitahi Gethenji.

Ndung’u na Gitahi ni wanawe Augustine Gethenji ambaye pia alikuwa ni mbunge wa zamani wa Tetu kabla ya kutangulia mbele ya haki miaka michache iliyopita.

Gitahi anadaiwa kuungana na baadhi ya wamiliki wa nyumba katika mtaa huo ulio na nyumba 55 za kifahari kutwaa udhibiti wa jumba la starehe mtaani humo (Bustani Bulding) lenye thamani ya Sh4 bilioni.

Katika jumba hilo la starehe, kuna kidibwi cha kuogelea, sehemu ya michezo, uwanda wa matembezi na kustarehe na madhari mazuri ya kubarizi.

Bw Nyaribo alimweleza hakimu kuwa ni kutokana na mzozo huu ambapo mbunge huyo wa zamani alikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Mashtaka dhidi ya Ndung’u hayakusomwa kuwezesha afisa anayechunguza kesi hiyo kuthibitisha iwapo washukiwa wengine wanne walioshtakiwa Jumanne walitoka kwa dhamana ndipo waagizwe wafikishwe kortini Oktoba 28, 2019.