HabariSiasa

Kikao cha Ruto na Kibwana chazua msisimko

April 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na PIUS MAUNDU

GAVANA wa Makueni Prof Kivutha Kibwana alipokutana na Naibu Rais William Ruto mnamo Jumanne, ilitarajiwa kikao hicho kiibue hali ya mshikemshike katika maeneo ya Ukambani.

Badala yake, viongozi katika Kaunti za Kitui, Machakos na Makueni wamepongeza mkutano huo katika ofisi ya Bw Ruto jijini Nairobi kama hatua sawa ya kisiasa na kuashiria kuwa eneo hilo liko tayari kumsikiliza mwanasiasa yeyote.

Mkutano huo umeibua gumzo kwani viongozi hao wawili walishikilia kuwa kikao hicho kilihusu suala la ushirikiano baina ya serikali za kaunti na ile ya kitaifa.

“Tulijadili maendeleo katika Kaunti ya Makueni na eneo zima la Ukambani. Miradi mikuu tuliyogusia ni pamoja na kuweka lami katika barabara ya Emàli-Ukia, bwawa la Thwake, mji wa kiteknolojia wa Konza Technocity, uwanja wa michezo wa Wote na miradi mingineyo,” ilisema taarifa aliyochapisha Prof Kibwana kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

“Tuna imani kwamba ushirikiano baina ya serikali ya kitaifa na za kaunti utawezesha ufanisi wa Ajenda Kuu Nne,” iliongeza taarifa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii ya Naibu Rais Ruto.

Mkutano huo ulifanyika siku moja baada ya Prof Kibwana, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha Wiper, kudokeza kuibuka kwa migawanyiko katika chama hicho. Kikao hicho kiliibua uvumi kwamba mazungumzo yao pia yaligusia siasa.

Maseneta Mutula Kilonzo Junior (Makueni) na Enock Wambua (Kitui) pamoja na wabunge Daniel Maanzo (Makueni), Patrick Makau (Mavoko) na Thaddeus Nzambia (Kilome) waliunga mkono mjadala wowote wa kisiasa uliofanyika.

Kwa mujibu wa viongozi hao, kikao hicho kilifanyika wakati mazungumzo baina ya Wiper na vyama vingine kuelekea 2022 yakikaribishwa.

 

Ni siasa tu

“Prof Kibwana na Naibu Rais William Ruto wote ni wanasiasa wa muda mrefu. Wanaodhania ni siasa tu zilizozungumziwa katika mkutano huo hawajakosea,” Bw Wambua aliambia Taifa Leo katika mahojiano na kuongeza kwamba hakufahamu masuala ya kisiasa yaliyojadiliwa kwenye kikao hicho.

“Ningeulizwa, ningewaambia (vigogo wa Wiper) waharakishe kukutana na Naibu Rais pamoja na viongozi wengine,” akaongeza Bw Kilonzo Jnr kuunga mkono matamshi ya viongozi wengine wa Wiper.

“Naibu Rais atakuwa mtu wa sawa kuingiliana na Wiper,” Bw Wambua alisema.

Wito kwa Wiper kujiweka pazuri kuunda miungano ya baada ya uchaguzi umezidi wakati chama hicho kikikabiliwa na changamoto za kutoka ndani na nje huku wachanganuzi wakisema misukosuko hiyo imeashiria Ukambani kuwa eneo lisilokuwa na misimamo mikali ya kisiasa.

Jumapili, Prof Kibwana alihimiza kinara wa chama Kalonzo Musyoka kudhibiti wanasiasa wasumbufu kutoka Ukambani ili kuweka chama hicho katika nafasi nzuri ya kuunda miungano na jamii nyinginezo.

Miongoni mwa wanasiasa hao ni Mbunge wa Mwingi ya Kati Gideon Mulyungi ambaye alimshambulia Gavana wa Kitui Charitu Ngilu kwa maneno makali wiki mbili zilizopita.