Kimataifa

Afisa wa zamani achunguzwa kwa mauaji ya halaiki Rwanda

July 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa

UFARANSA imeanza kumchunguza afisa mmoja wa zamani wa kijeshi wa Rwanda dhidi ya tuhuma kwamba alishiriki kwenye mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini humo mnamo 1994, ambapo zaidi ya watu 800,000 waliuawa.

Jumapili, viongozi wa mashtaka wa Ufaransa walisema uchunguzi dhidi ya Aloys Nyiwiragabo ulianza mara moja baada yake kupatikana akiwa amejificha viungani mwa mji wa Orleans.

Shirika la habari la kipekuzi la Ufaransa, Mediapart, pia lilishiriki kwenye harakati za kufichua mshukiwa alikokuwa amejificha.

Nyiwiragabo alihudumu kama mkuu wa ujasusi kwenye utawala wa Rais Juvenal Habyarimana.

Alitajwa na Mahakama ya Kitaifa ya Kuchunguza Mauaji ya Rwanda (ICTR), kama miongoni mwa watu wenye ushawishi walioshiriki na kupanga mauaji hayo dhidi ya Watutsi.

Licha ya kukamatwa kwake, serikali ya Rwanda, Ufaransa, Interpol na ICTR zilikuwa zimeondoa kibali cha kukamatwa kwake kilichotolewa miaka kadhaa iliyopita.

Kubainika kwa maficho ya mshukiwa kunajiri miezi miwili baada ya mshukiwa mwingine wa mauaji, Felicien Kabuga, kukamatwa viungani mwa Paris.

Kabuga alikamatwa baada ya kukwepa kukamatwa na polisi kwa zaidi ya miaka 25 katika nchi kadhaa. Anatuhumiwa kuwa miongoni mwa wafadhili wakuu wa mauaji hayo.

Tayari, ameomba kesi yake kuendeshwa Ufaransa, akidai “ataonewa” ikiwa atakabidhiwa serikali ya Rwanda.

Ufaransa imebainika kuwa ngome ya maficho kwa watu maarufu wanaotuhumiwa kushiriki kwenye mauaji hayo.

Maafisa wa uchunguzi wa Ufaransa wanaendesha mamia ya kesi za washukiwa wa mauaji hayo.

Mauaji yalianza baada ya ndege iliyokuwa imembeba Rais Habyarimana, ambaye alikuwa Mhutu kudunguliwa jijini Kigali Aprili, 6, 1994.

Ukatili huo uliwalenga Watutsi, ambao ni wachache na Wahutu wenye misimamo ya kadri.

Wakati huo huo, watu waliojihami Jumamosi waliwaua watu karibu 20 katika eneo la Darfur nchini Sudan, alisema Ibrahim Ahmad, ambaye ni afisa wa utawala eneo hilo.

Kulingana naye, wengi waliouawa ni wanawake na watoto. Waliuawa wakati wakiwa kwenye shughuli za kilimo kwenye mashamba yao.

Afisa alieleza kuna uwezekano mauaji hayo yalitokana na mzozo wa umiliki wa ardhi ambao umekuwa ukiendelea kwa muda mrefu miongoni mwa wenyeji.

“Miezi miwili iliyopita, serikali ilifanya kikao kati ya pande mbili husika ambapo ilikubaliwa kutakuwa na utaratibu wa kusuluhisha mzozo huo,” akasema, kwenye mahojiano na AFP.