Kimataifa

Ajabu bilionea akimwachia mbwa urithi wa Sh15.1 bilioni – pesa nyingi zaidi ya alizoachia familia

Na MASHIRIKA, WINNIE ONYANDO November 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

BILIONEA wa India Ratan Tata, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 86, amemwachia mbwa wake asilimia kubwa ya urithi wake.

Tata ambaye alikuwa mwenyekiti wa zamani wa kampuni ya Tata Group alimwachia mbwa wake (Tito) urithi wa Sh15.1 bilioni.

Kulingana na wosia wake, pesa hizo zingetumika kumlinda mbwa huyo aina ya German Shephered ambaye alikuwa rafiki wa dhati wa bwanyenye huyo.

Kama ilivyo desturi nchini India, mfanyabiashara huyo, ambaye hakuwahi kuoa au kupata watoto, angewaachia ndugu zake mali yake yenye thamani ya mabilioni, bilionea huyo alimwachia kaka yake, Jimmy Tata, na dada wa kambo Shireen na Deanna Jejeebhoy urithi pamoja na mfanyakazi, mpishi wake pamoja na mbwa wake.

Kulingana na wosia wa Tata, mbwa huyo alikuwa naye hadi dakika zake za mwisho duniani.

Jumla ya asilimia 80 ya mali yake imewekwa chini ya mbwa huyo, mfanyakazi na mpishi wake huku familia ikiachiwa asilimia 20 ya mali.

“Ndugu zake watarithi tu sehemu ya mali yake, isiyozidi pauni milioni 5,” sehemu ya wosia hiyo inasema.

Kulingana na rafiki wa karibu wa Tata, kiasi ambacho kimeachiwa mfanyakazi na mpishi wa zamani wa Tata, walio na umri wa miaka 50 na sasa wanamtunza Tito, ni hatua ya ukarimu mkubwa.

Kulingana na taarifa ya kituo cha habari cha Times of India, mbwa huyo alipelekwa kumpa heshima za mwisho bosi na rafiki yake kabla azikwe.

Inasemekana kuwa Tata alimwokoa mbwa huyo akizurura mitaani na akamchukua na kumfanya kuwa rafiki yake.