“Amani iwe nanyi nyote,” maneno ya kwanza ya Papa Leo XIV
AMANI iwe nanyi! Ndugu wapendwa, hii ndio ilikuwa salamu ya kwanza ya Kristo aliyefufuka, mchungaji mwema aliyeutoa uhai wake kwa watu Mungu. Mimi pia ningependa salamu hii ya amani iingie mioyoni mwenu, ifikie familia zenu na watu wote, popote walipo; na mataifa yote, na dunia yote: Amani iwe nanyi.
Hii ndiyo amani ya Kristo aliyefufuka, amani isiyo na silaha, ya unyenyekevu na ya kudumu. Inatoka kwa Mungu. Mungu ambaye anatupenda sote, bila mipaka wala masharti. Tuweke masikioni mwetu sauti dhaifu lakini daima ya ujasiri ya Papa Francis, aliyebariki Roma – Papa aliyebariki Roma na dunia siku ile ya asubuhi ya Pasaka.
Niruhusuni kuendeleza baraka hiyo hiyo. Mungu anatupenda, sisi sote, na uovu hautashinda. Sote tuko mikononi mwa Mungu. Bila hofu, tukiwa pamoja, mkono kwa mkono na Mungu na sisi kwa sisi, tutaendelea mbele. Sisi ni wanafunzi wa Kristo, Kristo yuko mbele yetu, na dunia inahitaji mwanga wake. Ubinadamu unamhitaji kama daraja la kumfikia Mungu na upendo wake. Ninyi hutusaidia kujenga madaraja kupitia mazungumzo na kukutana ili tuweze kuwa jamii moja daima katika amani.
Asante Papa Francis!
Asante kwa ndugu zangu Makadinali walionichagua kuwa Mrithi wa Petro na kutembea pamoja nanyi kama Kanisa lililo moja, tukitafuta pamoja amani na haki, tukifanya kazi pamoja kama wanawake na wanaume, waaminifu kwa Yesu Kristo bila hofu, tukimtangaza Kristo, kuwa wamishionari, waaminifu kwa Injili.
Mimi ni mwana wa Mtakatifu Augustino, Muagostino. “Pamoja nanyi mimi ni Mkristo, kwenu mimi ni askofu.” Hivyo basi na tuendelee kutembea pamoja kuelekea makao yale ambayo Mungu ametutayarishia.
Kwa Kanisa la Roma.Tunapaswa kutazama kwa pamoja jinsi ya kuwa Kanisa la kimishionari, kujenga madaraja, kufanya mazungumzo, daima kuwa wazi kuwapokea wote kwa mikono miwili, kama uwanja huu ulivyo wazi kwa wote, kwa wote wanaohitaji upendo wetu, uwepo wetu, mazungumzo yetu, upendo wetu.
[Kwa Kihispania]:
Shikamoo kwa wote na hasa kwa wale wa jimbo langu la Chiclayo huko Peru, watu waaminifu, wa kweli wanaosindikiza askofu na kumsaidia.
[Akirudi kwa Kiitaliano]:
Kwa ndugu zangu wote wa Roma, Italia, na wa ulimwengu mzima, tunataka kuwa Kanisa la kisinodi, linalotembea pamoja daima likitafuta amani, upendo, ukaribu – hasa kwa wale wanaoteseka.
Leo ni siku ya Supplicatio (Sala ya Maombi) kwa Mama Yetu wa Pompei. Mama yetu mbarikiwa Maria siku zote anataka kutembea pamoja nasi, kuwa karibu nasi, siku zote anataka kutusaidia kwa maombezi yake na upendo wake. Hivyo basi, tuombe pamoja kwa ajili ya utume huu, kwa ajili ya Kanisa lote, na kwa ajili ya amani duniani.
Tunaomba neema hii maalum kutoka kwa Maria, Mama yetu.