Kimataifa

Amerika yafunga ubalozi wake Ukraine shambulio jipya la Urusi likinukia

Na MASHIRIKA November 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

AMERIKA, Uhispania, Ugiriki na Italia ni kati ya mataifa ambayo Jumatano, Novemba 20, 2024 yalifunga ubalozi wao Ukraine kutokana na hofu ya kushambuliwa na makombora makali kutoka Urusi.

Hii ni baada ya Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu kushambulia Urusi Jumanne usiku. Ukraine ilipewa makombora hayo makali na Amerika ambayo iliipa idhini ya kuyatumia kwenye vita dhidi ya Urusi.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema makombora hayo yalilenga Bryansk ambalo ni eneo kwenye mpaka wao na Ukraine.

Makombora manane yalirushwa ambapo Urusi ilidai kuwa ililemaza makali ya matano na kuyaangusha huku kombora moja likilenga na kusababisha uharibifu ikiwemo kuanzisha moto kwenye makao ya jeshi.

Hata hivyo, Amerika ilisema kuwa Urusi ilidanganya kwani ilitibua na kuangusha tu makombora mawili yaliyorushwa na Ukraine.

Waziri wa Masuala ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov alishutumu Amerika kwa kuingilia vita kati vyao na Ukraine akisema wanastahili kulenga juhudi za amani.

Hapo jana, Italia ambayo pia inaunga Ukraine kwenye vita hivyo, ilisema kuwa itafunga ubalozi wake na shughuli zote zitaendeshwa kupitia mtandao wake wa kijamii.

Ubolozi wa Amerika uliwaambia wafanyakazi wake wasake hifadhi maeneo salama huku wakisema walikuwa wakitarajia Urusi ijibu mashambulizi ya Ukraine.

“Ubalozi wa Amerika unatoa tahadhari kwa raia wake wapate hifadhi eneo salama na ubalozi wetu umefungwa kwa muda,” ikasema taarifa ya Amerika.

Haya yanatokea wakati ambapo Urusi nayo ilidai kuwa imechukua usimamizi wa kijiji cha Illinka ambacho kipo mashariki mwa Ukraine.

Pia Urusi ilisema kuwa iliharibu droni 44 za Ukraine ambazo zilikuwa zikilenga miji ya Moscow, Novgorod, Kursk, Belgorod na Bryansk.

Jana asubuhi, droni sita ziliangushwa eneo la Samara kwa mujibu wa Gavana wa Kieneo, Vyacheslav Fedorishchev. Hata hivyo, hakukuwa na jeraha lolote au uharibifu ambao ulitokea.

Urusi imekuwa ikijigamba jinsi ambavyo imekuwa ikiangusha na kuharibu droni kutoka Ukraine kila siku.

Urusi pia imeyaonya mataifa wanachama wa Muungano wa NATO dhidi ya kusaidia Ukraine kwenye vita hivyo kwa kuipa silaha hatari.

Mkuu wa Kitengo cha Ujasusi dhidi ya mataifa ya kigeni, Sergey Naryshkin, alisema kuwa watalipiza kisasi iwapo NATO itaingilia vita hivyo na kuegemea Ukraine.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, Jumatano pia aliingilia mzozo huo akisema anapinga hatua ya Amerika kuruhusu Ukraine kutumia makombora hatari kuvamia Urusi.

Rais Erdogan alisema uamuzi huo unatishia kuwasha moto zaidi kwa kuwa mataifa mbalimbali yatachukua msimamo wao na kusaidia kila upande kijeshi.

Kiongozi huyo ametoa wito kwa Urusi na Ukraine kukomesha vita vyao ili kuepuka mauaji ya raia na uharibifu kwa sababu ubabe wa jeshi na silaha utadororesha tu uchumi na uthabiti wa nchi hizo.