Kimataifa

Amerika yafutilia mbali visa zote za raia wa Sudan Kusini

Na REUTERS, BENSON MATHEKA April 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

AMERIKA ilisema Jumamosi kwamba itafutilia mbali visa zote zinazomilikiwa na wanaomiliki pasipoti za Sudan Kusini kutokana na kushindwa kwa Sudan Kusini kuwapokea raia wake waliorejeshwa, huku hofu ikitanda barani Afrika  kwamba nchi hiyo inaweza kurudi vitani tena.

Utawala wa Rais wa Amerika Donald Trump umechukua hatua kali za kuimarisha utekelezaji wa sheria za uhamiaji, ikiwa ni pamoja na kuwarejesha makwao watu wanaoaminika kuwa Amerika kinyume cha sheria.

Utawala huo umeonya kwamba nchi zitakazoshindwa kuwapokea raia wao kwa haraka zitachukuliwa hatua, ikiwa ni pamoja na kuwekewa vikwazo vya visa au ushuru wa forodha.

Sudan Kusini imeshindwa kuheshimu kanuni kwamba kila nchi lazima ikubali kuwapokea raia wake kwa wakati mwafaka Amerika inapowarejesha, alisema Waziri wa Masuala ya Nje wa Amerika Marco Rubio katika taarifa.

“Kuanzia sasa, Idara ya Serikali ya Amerika ya Masuala ya Nje inachukua hatua za kufutilia mbali visa zote zinazoshikiliwa na watu wenye pasipoti za Sudan Kusini na kusitisha utoaji zaidi wa visa ili kuzuia kuingia kwao nchini Amerika,” alisema Rubio.

Ubalozi wa Sudan Kusini mjini Washington haukujibu mara moja ombi la kutoa maoni.

Wapatanishi kutoka Umoja wa Afrika waliwasili katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, wiki hii kwa mazungumzo yanayolenga kuzuia vita vipya vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo baada ya Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani wiki iliyopita.

Serikali ya Rais Salva Kiir imemlaumu Machar, mpinzani wake wa muda mrefu ambaye aliongoza uasi wakati wa vita vya 2013-2018 vilivyoua maelfu ya watu, kwa kujaribu kuchochea uasi mpya.

Kukamatwa kwa Machar kulifuatia wiki kadhaa za mapigano katika jimbo la Upper Nile kaskazini kati ya jeshi na wanamgambo wa White Army. Vikosi vya Machar vilikuwa na ushirikiano na White Army wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe lakini vinakanusha kuhusika nao kwa sasa.